logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Antonio Conte atimuliwa Tottenham baada ya kuwatusi wachezaji wake

"Sijazoea kuona hali ya aina hii. Naona wachezaji wengi wenye ubinafsi na sioni timu," alisema.

image
na Samuel Maina

Michezo27 March 2023 - 04:11

Muhtasari


  • •Tottenham ilitangaza kwamba meneja huyo mwenye umri wa miaka 53 ameondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.
  • •Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alidokeza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa ili kuweka klabu hiyo katika nafasi ya kushindana.

Tottenham imetamatisha mkataba na meneja wake Antonio Conte baada ya Muitaliano huyo  kuishambulia klabu na wachezaji wikendi iliyopita.

Jumamosi iliyopita, Antonio Conte ambaye amekuwa akiisimamia klabu hiyo yenye maskani yake London tangu Novemba 2021 aliwakashifu wachezaji wake akiwaita "wabinafsi" baada ya kutoka sare ya 3-3 na Southampton.

Siku ya Jumapili, Machi 26, Tottenham kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya klabu hiyo ilitangaza kwamba meneja huyo mwenye umri wa miaka 53 ameondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.

"Tunamshukuru Antonio kwa mchango wake na tunamtakia heri kwa siku zijazo," ilisomeka taarifa hiyo.

Kufuatia maendeleo hayo mapya, klabu hiyo ilitangaza kwamba Cristian  Stellini atachukua usukani hadi mwisho wa msimu huu wa 2022/23 na atasaidiwa na Ryan Mason kama kocha mkuu msaidizi.

Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alidokeza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa ili kuweka klabu hiyo katika nafasi ya kushindana.

"Tumebaki na mechi 10 za Ligi Kuu na tuna mapambano mikononi mwetu kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa. Sote tunahitaji kufanya kazi pamoja. Kila mtu anapaswa kujitokeza ili kuhakikisha mwisho wa juu zaidi kwa Klabu yetu na wafuasi wetu wa maana,  na waaminifu," Bw Levy alisema.

Antonio Conte anaondoka katika Tottenham baada ya kuiongoza kwa muda wa takriban miezi 16 kufuatia vijembe alivyowatupia wachezaji wake baada ya kutoka sare dhidi ya Southampton siku ya Jumamosi iliyopita.

"Sijazoea kuona hali ya aina hii. Naona wachezaji wengi wenye ubinafsi na sioni timu," alisema.

Aliongeza, "Sisi ni wachezaji 11 wanaoingia uwanjani. Ninaona wachezaji wenye ubinafsi, naona wachezaji ambao hawataki kusaidiana na hawaweki moyo wao."

Muitaliano huyo alisema wachezaji wa Tottenham wamezoea kutocheza kwa ajili ya kitu cha maana na hivyo hawana shida na matokeo duni.

"Hawataki kucheza kwa shinikizo, hawataki kucheza wakiwa na msukumo. Ni rahisi kwa njia hii. Hadithi ya Tottenham ni hii," alisema.

Kabla ya kusajiliwa Tottenham, Conte aliwahi kuwa meneja wa Chelsea, Inter Milan na Juventus.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved