Kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, Dele Alli ambaye anachezea Besiktas ya Uturuki kwa mkopo kutoka Everton ameibua sintofahamu kwenye mitandao ya kijamii baada yake kuonekana akiwa na puto mdomoni huku meza iliyokuwa mbele yake ikiwa imejaa aina mbalimbali za dawa kali, hasa Nitrous oxide, maarufu kwa jina la gesi ya kucheka.
Pia juu ya meza kulikuwa na vinywaji na chupa za maji pamoja na pakiti ya kadi za kucheza.
Alikuwa mahali hapo na marafiki zake kadhaa ambao hawakutambulika.
Picha hiyo ilionekana siku chache baada ya Alli kurejea England kutoka Uturuki ambako amekuwa kwa mkopo wa msimu mzima.
Ali amerejea England kwa ajili ya kuendelea na matibabu ya jeraha alilopata akiitumikia klabu hiyo ya Uturuki.
Ikumbukwe klabu ya Everton iliamua kumpeleka kwa mkopo Besiktas wakiwa na matumaini kwamba angeweza kufufua maisha yake ya soka lakini mambo yanaonekana kumwendea mbaya zaidi Uturuki
Dele Alli amekuwa na wakati mgumu sana klabuni hapo hali iliyopelekea kuwekwa benchi akituhumiwa kutohudhuria mazoezi na hata kuzomewa na mashabiki wa klabu hiyo.
Ilifikia hatua Besiktas walijaribu kusitisha mkataba wake wa mkopo lakini hawakuweza kwa sababu hakukuwa na kipengele cha kusitisha mkataba huo. Hata hivyo licha ya kurejea England Alli haruhusiwi kuichezea Everton kwa kuwa mkataba wake wa mkopo na timu hiyo ya Uturuki bado unaendelea.
Baada ya mkataba huo wa mkopo, Everton inatarajiwa kufikiria iwapo itamruhusu kusalia katika klabu hiyo hadi mkataba wake wa sasa na klabu hiyo utakapomalizika 2024 au kusitisha mkataba kabla ya msimu wa 2023-2024 kuanza.
Alli alisifiwa kama mmoja wa wanasoka wa kutumainiwa wa England lakini amekuwa na shida uwanjani tangu alipoondoka Tottenham Januari mwaka jana.