Vita kati ya magiwiji wawili wa soka duniani katika karne ya sasa Christiano Ronaldo na Messi iko mbali sana na kutamatika.
Hii ni baada ya Ronaldo kumpiga mkwara mzito mwenzake Messi siku moja tu baada ya kutambulishwa kama mchezaji wa Inter Miami inayoshiriki ligi ya Marekani, MSL.
Ronaldo katika mahojiano na vyombo vya habari nchini Ureno, alijitapa kwamab ni yeye amechangia katika kuwashawishi wachezaji wengi kutoka ligi mbali mbali kuelekea katika ligi ya Saudia, ikiwa ni miezi saba tu tangu atue katika klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia.
Ronaldo alisema kwamba ligi ya Saudi kufikia sasa ni bora Zaidi kuliko ile ya MSL alikoenda kucheza Messi.
“Ligi ya Saudi ni BORA kuliko MLS,” alisema Ronaldo, alilenga kumshambulia Messi kwa njia fiche.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alikiri kwamba yeye alishamaliza kibarua chake katika ligi za Ulaya, akisema kuwa ligi hizo zimeshuka katika viwango vya mchezo, isipokuwa tu ligi ya Premia nchini Uingereza.
“Sitarudi kwenye soka la Ulaya, sahau - mlango umefungwa kabisa. Nina umri wa miaka 38, pia soka la Ulaya limepoteza ubora mkubwa... moja tu halali ni Premier League, wako mbele zaidi ya ligi zingine zote,” Mreno huyo alisema.
Pia alizungumzia ushawishi wake kwa wachezaji wengi akisema kwamba kila aendapo huvutia wengi kumfuata akitolea mfano alipoenda Juventus ya Italia na kuifufua ligi hiyo, jambo sawia ambalo amesababisha katika ligi ya Saudia.
“Nina uhakika 100% sitarejea katika klabu yoyote ya Ulaya. Nilifungua njia ya kuelekea ligi ya Saudia... na sasa wachezaji wote wanakuja hapa. Katika mwaka mmoja, wachezaji wengi zaidi na zaidi watakuja Saudi. Nilipojiunga na Juventus, Serie A ilikuwa imekufa na kisha baada ya kusaini… ikafufuliwa. Popote Cristiano anapoenda anazalisha maslahi ya juu,” alijipiga kifua.
Mchezaji huyo alimaliza kwa kutabiri kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, ligi ya Saudia itakuwa bora na juu kwa viwango vya mchezo kuliko ligi ya Uuturiki na Uholanzi.
“Walinikosoa kwa kuja kwenye Ligi ya Saudi, lakini nini kilifanyika sasa? Nilifungua njia... na sasa wachezaji wote wanakuja hapa. Katika mwaka mmoja, wachezaji wengi zaidi na bora watakuja Saudi. Katika mwaka mmoja ligi ya Saudi itapita ligi ya Uturuki na ligi ya Uholanzi,” alisema kwa madaha mengi.