Kocha wa Manchester City Pep Guardiola anatazamiwa kukosa mechi mbili zijazo za timu yake baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.
Guardiola, 52, alikuwa akisumbuliwa na kile City walisema kuwa ni "maumivu makali" ya mgongo na alisafiri hadi Barcelona kwa ajili ya "operesheni ya dharura" lakini "ndogo".
City itacheza na Sheffield United siku ya Jumapili na kuwakaribisha Fulham tarehe 2 Septemba katika Uwanja wa Etihad.
Guardiola anatarajiwa kurejea kazini baada ya mapumziko.
Meneja Msaidizi Juanma Lillo atachukua nafasi ya mazoezi ya kikosi cha kwanza.
City ilisema operesheni hiyo, iliyofanywa na Dkt Mireia Illueca, ilikuwa ya "mafanikio" na kuwa "atapona na kurejea Barcelona".
Taarifa hiyo iliongeza: "Kila mtu katika Manchester City anamtakia Pep ahueni ya haraka, na anatazamia kumuona akirejea Manchester hivi karibuni."
Guardiola aliiongoza klabu hiyo kutwaa Ligi Kuu, Kombe la FA na taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. City wanashika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Premia katika hatua za mwanzo, wakiwa sawa kwa pointi sita na vinara Brighton na Arsenal katika nafasi ya tatu, baada ya kuwalaza Burnley na Newcastle katika michezo yao miwili ya ufunguzi.