Kwa mara ya kwanza katika historia ya mataifa matatu ya Afrika Mashariki, mashindano ya kandanda ya bara yatafanyika kwa pamoja katika ukanda huu na Kenya, Tanzania na Uganda watakuwa wenyeji wa shindano hilo kubwa la kambumbu barani.
Jitihada za pamoja za nchi hizo tatu kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ziliidhinishwa na mawasiliano kufanywa Jumatano.
Lakini kuna faida gani za kuandaa mashindano ya AFCON?
Hizi hapa ni baadhi ya faida ambazo zinakuja na taifa kuteuliwa kuandaa mashindano hayo;
Uhitimu otomatiki kwa timu za taifa mwenyeji
Tanzania imecheza katika michuano miwili ya AFCON - mwaka wa 1980 na 2019. Uganda ndiyo taifa lenye mafanikio makubwa zaidi la Afrika Mashariki katika mashindano ya AFCON. Nchi hiyo imeshiriki katika mashindano saba ya AFCON.
Mwaka 1978, taifa hilo la Afrika Mashariki lilikuwa mshindi wa pili, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ghana katika fainali za AFCON zilizochezwa kwenye Uwanja wa Accra Sports nchini Ghana. Mara nyingine Uganda imeshiriki AFCON ni 1962, 1968, 1974, 1976, 2017 na 2019.
Kenya imejitokeza katika michuano sita ya AFCON - mwaka wa 1972, 1988, 1990, 1992, 2004 na 2019. Nchi hiyo haijawahi kusonga mbele zaidi ya hatua za makundi.
Sasa kwa vile mataifa hayo matatu yataandaa kwa pamoja michezo ya AFCON 2027, yataepushwa na changamoto ya kufuzu kupitia mechi za awali.
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) linasema kwenye tovuti yake kwamba mataifa mwenyeji "yanafuzu moja kwa moja kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika."
Mataifa ambayo yamefuzu kwa michezo ya AFCON hupokea takriban $600,000 {Milioni 88.8 pesa za Kenya} kila moja kama pesa taslimu. Timu nne za juu, hata hivyo, hupata pesa zaidi.
Sekta ya utalii ya taifa mwenyeji hupigwa jeki pakubwa
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa kila taifa linapoandaa mashindano makubwa kama vile AFCON, kunakuwa na matokeo chanya katika sekta ya utalii nchini. Jambo hilo linajulikana kama utalii wa michezo.
Katika utafiti wa Februari 2023 uliochapishwa na Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini ukichambua athari za utalii za zabuni ya ukaribishaji wa Cameroon 2022, waandishi Siyabulela Nyikana na Tembi Tichaawa wanasema: "Kumbukumbu za kudumu za maeneo ya ndani zinaweza kusababisha kutembelea tena na hivyo kukuza idadi ya watalii wa ndani.”
Wakati Misri ilipoandaa AFCON 2019, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilisema sekta ya utalii ya taifa hilo la Afrika Kaskazini iliimarishwa mara kadhaa kutokana na mashindano hayo. Mapato yaliyohusishwa na mashindano hayo pekee yalifikia $83 milioni.
Nchi 24 (24) zinashiriki michezo ya AFCON. Hii inamaanisha kuwa makumi, ikiwa sio mamia ya watu, husafiri na timu zao hadi taifa mwenyeji.
Wafanyakazi wa vyombo vya habari, makampuni ya udhamini, wapenzi wa soka, na watalii wa kigeni humiminika katika nchi mwenyeji kwa ajili ya hafla hiyo, na hivyo kukuza utalii wa ndani.
Utalii, hasa wanyamapori, ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa Kenya, Uganda na Tanzania. Mataifa yatatumaini kunufaika na idadi kubwa ya watalii mwaka wa 2027 ili kupata mapato zaidi kutokana na ziara za AFCON.
Nafasi ya viwanja vya taifa mwenyeji kupata maboresho mapya
Ili taifa lifuzu kuandaa michuano ya AFCON, ni sharti lifikie viwango vilivyowekwa na CAF.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linataka nchi itakayoandaa AFCON, au nchi, lazima ziwe na angalau viwanja sita, vikiwa na viwili vinavyoweza kubeba mashabiki wasiopungua 40,000, vingine viwili vinavyoweza kubeba mashabiki 20,000, na viwili vinavyoweza kubeba mashabiki wasiopungua 15,000.
Kabla ya haki za uenyeji kugawiwa taifa fulani, CAF hutuma maafisa wake kutathmini ubora wa viwanja vyake.
Hii ina maana kwamba ikiwa taifa lilikuwa na viwanja vya chini vya viwango hapo awali, ingelazimika kuzirekebisha au kuziboresha ili kufikia viwango vya CAF.
Kwa muda mrefu, hii inahakikisha kwamba nchi inakuwa na viwanja vya ubora, hata baada ya kuandaa mashindano.
Kenya imetangulia mbele ya Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Moi Kasarani (zote mbili katika mji mkuu Nairobi) na Uwanja wa Kipchoge Keino katika mji wa Bonde la Ufa wa Eldoret kama viwanja vya kutumika katika michezo ya AFCON 2027.
Tanzania itatumia Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa na pengine Uwanja wa Azam Sports Complex, zote zilizo katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam, kwa ajili ya michuano ya AFCON.
Uganda, kwa upande mwingine, itatumia Uwanja wa Taifa wa Nelson Mandela, Namboole, katika mji mkuu wa Kampala, wenye uwezo wa kubeba watu 45,000 kwa michezo hiyo.
Mataifa hayo matatu yalianza kukarabati uwanja huo baada ya kuwasilisha ombi lao la kuandaa AFCON mwezi Mei.
Miundombinu iliyoboreshwa
CAF inazitaka nchi wenyeji lazima waweke mazingira salama wakati wa kuandaa michezo ya AFCON.
Hii mara nyingi huwalazimu wenyeji kuboresha mitandao ya barabara, taa za barabarani na miundombinu ya mawasiliano.
Kwa mfano, wakati Cameroon ilipoandaa AFCON ya 1972, nchi hiyo ilishuhudia uboreshaji mkubwa katika viwango vyake vya viwanja na miundombinu inayoambatana, ambayo ilinufaisha nchi kwa miaka mingi ijayo, Nyikana na Tichaawa wa Chuo Kikuu cha Johannesburg wanasema katika utafiti wao.
Miaka ya upangaji na uwekezaji inaona mataifa mwenyeji yakiweka kiasi kikubwa cha bajeti zao kwa maendeleo ya miundombinu na urekebishaji wa huduma za kijamii.
Taifa mwenyeji hujizolea umaarufu kwa Wasifu wake
Kuna ushahidi wa kimaadili unaopendekeza kwamba mataifa ambayo huandaa matukio ya kikanda, bara au kimataifa yanafurahia sifa iliyoboreshwa ya kimataifa.
Utafiti wa 2010 uliofanywa na Geir Gripsrud na Erik Nes wa BI Norwegian Business School unaonyesha kuwa taswira ya nchi inaweza kubadilishwa kwa kuandaa matukio ya kimataifa, na vipimo vya taswira ya nchi kwa upande mwingine "huhusiana na taswira ya bidhaa na nia ya kitabia kuhusu ununuzi wa bidhaa na utalii. "
Waandishi hao wawili, hata hivyo, walisisitiza kwamba "usimamizi sahihi" wa michezo ya kimataifa ndiyo njia pekee ya uhakika ya kuboresha wasifu wa kimataifa wa nchi mwenyeji.
"Hakuna hakikisho kwamba taswira ya nchi mwenyeji itaboreka. Inaweza kuharibika," walisema katika utafiti wao.