Ligi ya vilabu vya soka barani Afrika, kwa kimombo African Football League itang’oa nanga nchini Tanzania kuanzia Ijumaa ya Oktoba 20.
Ligi hiyo itazinduliwa katika uwanja wa kimataifa wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza na itajumuisha vilabu 8 vikiwemo Simba SC ya Tanzania, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, miamba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, TP Mazembe, Petro Atletico de Luanda ya Angola, Esperance ya Tunisia, Al Ahly ya Misri, Enyimba ya Nigeria na Wydad ya Morocco.
Mechi ya kwanza itakuwa katika uwanja huo kati ya wenyeji Simba SC na miamba wa soka wa Misri Al Ahly, ambapo imearifiwa tayari Wamisri wametua nchini Tanzania japo kwa kimya kimya wakiwa wamejihami na kila kitu ikiwemo vyakula vyao.
Ripoti nchini Tanzania zimesisitiza kuwa Wenger atagusa msingi nchini humo siku ya Alhamisi, wakati muafaka wa tukio hilo. Pia imeripotiwa kuwa huenda Rais wa FIFA Gianni Infantino atapamba hafla hiyo nchini Tanzania.
Shindano hilo lilizinduliwa mwaka jana, likiwa na zawadi ya dola milioni 4 kwa washindi.