Kocha wa timu ya taifa, Harambee Stars Engin Firat amefichua kwamba ana mpango wa kikosi chake kushiriki mchezo wa kirafiki na timu za taifa za Italia na pia Ufaransa.
Katika mahojiano na gazeti la People Daily, Firat alisema kwamba wengi huenda wakapuuzilia mbali ndoto hiyo wakisema kuwa ni hekaya za Abunuwasi lakini yeye yuko imara na atasukuma hai ahakikishe ombi lake kwa Italia na Ufaransa limeitikiwa.
“Ninapanga kupata mechi dhidi ya timu kubwa, pengine mabingwa wa zamani wa dunia Ufaransa au Italia. Watu wengine wanaweza kudhani ni ndoto tu, lakini kupitia mawasiliano yangu ya karibu, itafanyika, " alisema Firat.
Wakati wengi wanakejeli ndoto hiyo, ni vizuri kukumbuka kwamba raia huyo wa Uturuki tangu achukue mikoba ya kuiongoza Harambee Stars amewezesha timu hiyo kushiriki mechi za kirafiki dhidi ya timu za mataifa mahiri ikiwemo Urusi, Qatar, Iran na nyingine.
Wakati huo huo pia ni vyema kujua kwamba timu za taifa za Italia na Ufaransa ni timu mahiri ambazo zimeboreshwa kwa muda mrefu na hata kushinda mataji katika mashinandano makubwa ikiweo Euro na kombe la dunia.
Mnamo Novemba 18, 2023, Ufaransa, mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia (1998 na 2018) ambao walipoteza kidogo fainali ya 2022 kwa Argentina kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi, walipambana na Gibraltar katika mechi ya kufuzu kwa Euro 2024.
Ufaransa ilitawala mechi hiyo, na kupata ushindi mnono wa mabao 14-0 dhidi ya Gibraltar, timu ambayo kwa sasa imeorodheshwa katika nafasi ya 198 na FIFA.
Je, unadhani Kenya itang’oka kwenye kucha za Ufaransa endapo Firat atatimiza ndoto hiyo?