Meneja wa Liverpool, Mjerumani Jurgen Klopp amewapiga vijembe wachezaji wawili wa Chelsea, Moises Caicedo na Romeo Lavia kwa kuikataa Liverpool msimu uliopita wa joto.
Liverpool walikuwa na nia kubwa ya kutaka kumsajili kiungo mkabaji baada ya kuwapoteza Fabinho na nahodha Jordan Henderson kwenye Ligi Kuu ya Saudia.
Katika orodha yao walikuwa na wachezaji Moises Caicedo kipindi hicho akitumikia Brighton na Romeo Lavia akitumikia Southampton na mpaka maelewano yakaafikiwa baina ya timu lakini wachezaji wote wkaikataa Liverpool na badala yake kuichagua Chelsea.
Sasa baada ya Chelsea kuonyesha viwango duni kimchezo na Liverpool kuimarika pakubwa hadi kuketi katika nafasi ya kwanza kwenye jedwali baada ya mzunguko wa raundi ya 16 ya EPL, kocha Klopp amewakejeli wawili hao kwa kuikataa The Reds na kutimukia The Blues.
"Majira ya joto tuliyokuwa nayo, tulikuwa na mambo machache ya ajabu katika soko la uhamisho, lakini hapa kati yetu, naweza kusema, 'Mungu wangu, tulikuwa na bahati, eh?'. Tuligundua kuwa viungo wengine wa kati hawakutaka kujiunga na Liverpool; unaona kilichotokea," Klopp alisema kama ilivyonukuliwa na This is Anfield.
Liverpool hatimaye ilimsajili Wataru Endo kutoka Stuttgart na tangu wakati huo wamekuwa wapinzani wa taji. Kwa sasa wanaongoza jedwali la Premier League wakiwa na pointi 37, pointi moja mbele ya Arsenal.
Chelsea, wakati huohuo wako katika nafasi ya 12 baada ya kuambulia kipigo cha saba msimu huu katika mchezo wa kunyenyekea wa 2-0 dhidi ya Everton.