Waziri wa michezo wa Kenya, Ababu Namwamba amewapigia upatu mkubwa Taifa Stars ya Tanzania kushinda mashindano ya AFCON Makala ya mwaka huu yanayoendelea nchini Ivory Coast.
Wakati wa uchambuzi wake kwenye kituo cha utangazaji cha taifa la Kenya mnamo Jumatano, Januari 17, Namwamba alidai kuwa awali Taifa Stars ilichukuliwa kuwa moja ya timu dhaifu zaidi katika michuano hiyo, inaweza kusababisha taharuki na kutwaa ubingwa.
Namwamba alisema, “Chochote kinawezekana katika soka. Ikiwa historia ya hivi karibuni imetufundisha chochote, ni kwamba hakuna watu wa chini kwenye soka. Mimi ni Afrika Mashariki. Mwana Afrika Mashariki ndani yangu unaisisitiza Tanzania, nikiwaambia, naamini mnaweza kupigana vizuri.”
Waziri huyo alisema kwamba Makala ya mwaka huu yamemfunza kwamba hakuna mnyonge katika michuano hiyo, akirejelea jinsi timu za mataifa yaliyochukuliwa kuwa wanyonge zilivyoshangaza timu za mataifa yaliyochukuliwa kuwa wababe wa soka.
“Hakuna mnyonge, yeyote anaweza kushinda AFCON, ikiwemo Tanzania,” Ababu alisisitiza.
Hata hivyo, Taifa Stars iliambulia kichapo cha mabao 3-0 mikononi mwa Morocco ambao walifikia hatua na nusu fainali katika Makala ya kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
Ababu alisema kwamba kama ambavyo wengi wanawaona Tanzania kuwa wanyonge, wegni waliona Morocco kuwa wanyonge wakati wa kombe la dunia lakini waliishia kuwashangaza wengi kwa kufika nusu fainali.
"Kila mtu anaweza kushinda kila mtu. Hakuna aliyeipa Morocco nafasi wakati wa Kombe la Dunia nchini Qatar, lakini walikwenda hadi nusu fainali. Hakuna kinachozuia Tanzania kufanya vyema,” alisema Waziri wa Michezo.