Takriban wachezaji saba wa timu ya taifa ya Algeria, akiwemo nahodha Riyad Mahrez wanaripotiwa kuwaza kustaafu kufuatia tukio la kushtukiza la kubanduliwa kutoka katika michuano ya Afcon 2023
The Desert Warriors walishindwa kufuzu kwa hatua ya 16 bora baada ya kumaliza wa mwisho katika Kundi D la michuano hiyo inayoendelea nchini Ivory Coast.
Mchezo wao wa mwisho wa Algeria ulikuwa dhidi ya Mauritania siku ya Jumanne usiku walipopoteza kwa kushtukiza 0-1 dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Walibanduliwa nje ya michuano hiyo bila ushindi wowote baada ya awali kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Burkina Faso na 1-1 dhidi ya Angola.
Katika mechi ya fainali, Mahrez ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaoripotiwa kuwaza kustaafu, aliwekwa kwenye benchi na meneja, Djamel Belmadi licha ya umuhimun wa mchuano huo. Hii hata hivyo haikuisha vyema kwa Wanajangwani hao ambao walichapwa na kubanduliwa nje ya michuano hiyo.
Licha ya kunyanyua taji hilo la kifahari la Afrika takriban miaka mitano iliyopita, vijana wa Djamel Belmadi hawakufanikiwa kufuzu kutoka katika hatua ya makundi.
Mahrez, ambaye aliichezea Algeria mechi yake ya kwanza mwaka 2014 na kuiongoza kushinda AFCON 2019, sasa anasemekana kuwa yuko tayari kuiaga timu hiyo ya taifa baada ya miaka 10 kufuatia kuondolewa kwao kutoka kwa michuano hiyo.
Mbali na mshambulizi Riyad Mahrez, wachezaji wengine sita wa timu ya taifa nao wanaripotiwa kuamua kustaafu kucheza soka la kimataifa baada ya Wanajangwan kuondolewa kwenye michuano hiyo. Sita hao ni pamoja na Sofiane Feghouli, Aïssa Mandi, Raïs M’Bolhi, Nabil Bentaleb, Baghdad Bounedjah na Youcef Belaïli.
Kando na wachezaji saba wanaoripotiwa kustaafu, kocha Djamel Belmadi pia amekubali kujiuzulu baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika siku ya Jumanne, shirikisho la soka nchini humo lilisema Jumatano.
Belmadi alikuwa amewaambia wachezaji wake kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwamba angeacha kazi baada ya Algeria kuchapwa 1-0 na Mauritania na amekubali kusitisha mkataba wake, rais wa shirikisho la Algeria Walid Sadi alisema.
"Nilikutana na kocha wa kitaifa ili kujadili matokeo ya kuondolewa kwa uchungu huu, na tukafikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake. Tunamshukuru kocha kwa yote aliyoifanyia timu na tunamtakia mafanikio mema katika maisha yake yote,” Sadi alisema.