Klabu ya soka ya Uingereza, Chelsea imeingia katika mkataba na taifa jirani la Tanzania mahususi kwa kunadi utalii wa kisiwa chake cha Zanzibar, gazeti la The Citizen limeripoti.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utalii wa kisiwa cha Zanzibar sasa unatarajiwa kuimarika zaidi baada ya serikali ya Zanzibar kushirikiana na klabu ya soka ya Uingereza Chelsea katika makubaliano ya utangazaji.
Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi akiwakaribisha Mkuu wa Kitengo cha Mauzo wa Chelsea FC Barnes Hampel na ujumbe wake Ikulu mjini Zanzibar Februari 1, 2024.
Mkutano huo na Chelsea ulilenga katika kukuza sekta ya utalii Zanzibar na kukuza maendeleo ya soka katika visiwa hivyo, ambayo ni pamoja na uanzishaji wa vyuo vya soka ndani ya Visiwa hivyo.
Bw Hampel na timu yake wanatarajiwa kuendelea na ziara yao ya Tanzania kwa kusafiri kuelekea bara Wikendi hii.
Ratiba yao ni pamoja na kukutana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro, kujadili mipango ya maendeleo ya michezo.
Kisha wanalenga kupata hadhira na Rais Samia Suluhu Hassan, kama ilivyothibitishwa na mratibu wa Chelsea FC nchini Tanzania, Bw. Mohamed Reza Saboor.
Hatua ya Chelsea FC kukubali kunadi utalii wa Zanzibar inakuja wakati ambapo timu zingine kama Arsenal na Bayern Munichen zikiwa katika mikataba ya kunadi utalii wa Rwanda.