Wanasoka wa zamani nchini Kenya wametoa wito kwa uongozi wa shirikisho la soka nchini FKF kutoa nafasi kwa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kusimamia chaguzi zake ambazo zinatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka juu.
Jumatano, muungano wa wanasoka wa Kenya, KeSPA uliitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai kwamba ili kuwepo kwa uwazi katika chaguzi zote za shirikisho la FKF kutoka ngazi za mashinani hadi kitaifa, ni sharti IEBC iratibiwe kusimamia uchaguzi huo.
Muungano huo unaoongozwa na mwanasoka wa zamani Harold Ndege alisema kwamba iwapo uchaguzi huo utafuata kanuni kama zile zilizotumika katika uchaguzi wa 2020, basi wawaniaji wengi watafungiwa nje na hivyo kuwapa kazi rahisi viongozi wa sasa wa FKF wakiongozwa na rais wa shirikisho, Nick Mwendwa.
“Kanuni za uchaguzi za FKF za 2020 zinasema kwamba katibu wa FKF anaweza kuhudhuria mkutano wa kamati ya upigaji kura katika nafasi ya mshauri bila kura. Hii ni muingiliano wa matakwa ndani ya uongozi wa sasa wa FKF,” Ndege alisema kwa sehemu.
Ndege pia alisema kwamba takwa la mwaniaji katika kanuni hiyo ya 2020 iliyopitishwa Januari mwaka huu kutumika katika uchaguzi wa Oktoba linafaa kutupiliwa mbali.
Katika mkutano huo na wanahabari, Ndege alikuwa ameongozana na mshambuliaji wa zamani wa Harambee Stars Dennis Oliech, mwanasoka wa zamani Frank Ogolla na refa wa FIFA mstaafu David Gikonyo.