Rais wa klabu ya Napoli ya Italia, Aurelio De Laurentiis amefunguka kwamba huenda mchezaji wao nyota, Victor Osimhen akawekwa sokoni katika dirisha la uhamisho majira ya joto.
De Laurentiis aliweka wazi kwamba mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Nigeria atakuwa anauzwa kwa kati ya Euro milioni 120 hadi 130 na kutahadharisha klabu yoyote inayomtaka kwamba hawatakuwa tayari kupunguza hata euro moja.
Osimhen ambaye amekuwa wa moto katika misimu miwili iliyopita kwa Napoli amekuwa akilengwa pakubwa na timu ya Chelsea ambao sasa wametakiwa kujihami na euro milioni 130 – sawa na bilioni 20 pesa za Kenya ili kuipata saini yake.
Mnigeria huyo mwenye umri wa miaka 25 yuko juu kwenye orodha fupi ya washambuliaji wa The Blues msimu huu wa joto wakitaka kuimarisha safu yao ya ushambuliaji baada ya msimu mbaya wa 2023/24.
Kulingana na Score Nigeria, Napoli wako tayari kumuachilia Osimhen lakini hawatakubali ila kipengele chake kamili cha kuachiliwa iwapo wataachana na mshambuliaji huyo wa Super Eagles katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Mshambulizi huyo wa Nigeria hivi majuzi alisaini nyongeza ya mkataba na mabingwa hao watetezi wa Serie A hadi 2026, ambayo Rais Aurelio De Laurentiis alithibitisha kuwa ina kifungu kikubwa cha kuachiliwa kwake.
Arsenal na Paris Saint-Germain ni vilabu vingine viwili vinavyoripotiwa kumtaka Osimhen huku The Gunners wakimtaka nyota huyo wa Napoli kuongoza safu yao ya ushambuliaji msimu ujao, huku PSG wakimtaka kuchukua nafasi ya Kylian Mbappe anayeondoka.