Mshambulizi matata wa Uingereza Bukayo Saka ameondoka kwenye kambi ya timu ya taifa na kurejea katika klabu yake ya Arsenal.
Timu ya taifa ya Uingereza, The Three Lions ilithibitisha kuondoka kwa Bukayo Saka siku ya Alhamisi jioni na kueleza kuwa alirejea Emirates kuendelea na matibabu.
Katika taarifa yake, timu ya taifa hilo ilithibitisha kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 aliripoti kambini akiwa na jeraha na hivyo ameshindwa kufanya mazoezi.
"Bukayo Saka ameondoka kwenye kambi ya Uingereza na kurejea katika klabu yake kwa ajili ya kuendelea na matibabu," The Three Lions ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya timu ya taifa.
Taarifa hiyo ilisema zaidi, "Mshambuliaji huyo wa Arsenal aliripoti St. George's Park akiwa na jeraha na ameshindwa kushiriki katika mazoezi. "
Timu hiyo ambayo inasimamiwa na kocha Gareth Southgate hata hivyo ilibainisha kuwa hakutakuwa na mchezaji mwingine atakayeitwa kuchukua nafasi ya mshambulizi huyo wa Arsenal huku wakijiandaa kumenyana na Brazil na Ubelgiji katika siku zijazo.
"Hakuna mbadala mwingine unaopangwa wakati kikosi cha wachezaji 25 cha England kikiendelea na maandalizi ya mechi zijazo za kimataifa na Brazil na Ubelgiji," taarifa hiyo iliongoza.
Bukayo Saka amekuwa kiungo muhimu sana ya timu ya taifa ya Uingereza tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2020. Kipaji chake kikubwa na jukumu muhimu limemfanya kutawazwa mchezaji bora wa mwaka wa Uingereza kwa miaka miwili mfululizo.
Sio kwa England pekee, pia amekuwa muhimu sana kwa klabu yake ya Arsenal, huku akiisaidia kumaliza katika nafasi ya pili msimu wa EPL 2022/23, na pia akiwa amefunga mabao kadhaa na kuisaidia kuwa kileleni mwa jedwali la EPL 2023.