Klabu ya soka ya KCB inayoshiriki kwenye ligi kuu ya FKF humu nchini imetangaza kudukuliwa kwa akaunti yao ya Facebook.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, KCB walifahamisha umma kwamba akaunti hiyo haipo mikononi mwao bali imeshikiliwa na wadukuzi.
Waliahidi kwamba mchakato unaendelea wa kuikomboa.
“Tunasikitika kuwataarifu mashabiki wetu wa nguvu kwamba akaunti yetu ya Facebook imedukuliwa. Tunaendelea kutia juhudi ili kuirejesha mikononi mwetu. Kwa wakati huu, tunawaomba mashabiki wetu kupuuzilia mbali mambo yote yanayochapishwa kwenye ukurasa huo,” sehemu ya ripoti ilisema.
Katika uangalizi wa haraka, tulibaini kwamba ukurasa huo kwa kipindi cha kama saa 24 hivi umekuwa ukifurikwa na machapisho ya picha na video sa watu wazima.
Itakumbukwa miezi kadhaa iliyopita, klabu ya Shabana pia ilitangaza kudukuliwa kwa ukurasa wao wa Facebook ambao mpaka sasa haujawahi rejeshwa mikononi mwao licha ya juhudi nyingi kuendelea.
Mwaka jana, ukurasa wa chuo kikuu cha Kabarak pia ulidukuliwa na kutumiwa na kijana raia wa kigeni kwa Zaidi ya wiki moja kabla ya chuo hicho kuurejesha mikononi mwao.