Kocha mkuu wa Manchester United, Erik ten Hag amejibu madai yanayoenezwa kwamba huenda akafutwa kazi katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Akizungumza mbele ya kurejea kwa michuano ya wikendi baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha michuano ya kirafiki ya kimataifa, ten Hag alisema kwamba yeye na wachezaji wake hawajali kuhusu uvumi huo.
Meneja huyo Mholanzi alisema kwamba amezoea uvumi kama huo kwani mtu unapofanya kazi katika klabu kubwa kama Manchester United, ni kawaida kusikia uvumi huo na hivyo yeye na wachezaji wake wamekwisha jifunza kutoyatilia maanani kw asana.
“Lengo langu liko kwenye mchakato, ni kucheza katika kiwango bora na kukuza wachezaji - sio uvumi wa waandishi wa habari".
"Ni Manchester United na daima kutakuwa na kelele karibu na klabu, timu, meneja na wachezaji. Unapofanya kazi kwenye soka la juu, unaizoea. Kwa hiyo hatujali. Wachezaji hawajali. sijali”.
"Tuko pamoja kwenye boti na tunajua lazima tufanye na kupata matokeo sahihi kwa Man United,” ten Hag alisema.
Manchester United watashuka dimbani alasiri ya Jumamosi kucheza dhidi ya Brentford.