logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Marcus Rashford avunja kimya baada ya kutemwa nje ya kikosi cha Uingereza

Kikosi hicho hata hivyo kitapunguzwa hadi wachezaji 25 kabla ya kuanza kwa Euro 2024 mnamo Juni.

image
na Samuel Maina

Michezo22 May 2024 - 12:16

Muhtasari


  • •Rashford alikuwa na matashi mema Southgate hata baada ya jina lake kutojumuishwa kwenye kikosi cha mazoezi ya Pre-Euro 2024.
  • •Kikosi hicho hata hivyo kitapunguzwa hadi wachezaji 25 kabla ya kuanza kwa Euro 2024 mnamo Juni.

Mshambulizi wa Manchester United Marcus Rashford alikuwa na matashi mema kwa timu ya soka ya Uingereza hata baada ya jina lake kutojumuishwa kwenye kikosi cha mazoezi ya Pre-Euro 2024.

Siku ya Jumanne, kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Gareth Southgate alitoa orodha ya wachezaji 33 ambao watakuwa kwenye kambi ya mazoezi na Marcus Rashford hakuwa miongoni mwao.

Katika orodha rasmi ya kikosi cha mazoezi iliyotolewa, Southgate aliwachagua Jude Bellingham, Jarrod Bowen, Eberechi Eze, Phil Foden, Anthony Gordon, Jack Grealish, Harry Kane, James Maddison, Cole Palmer, Bukayo Saka, Ivan Toney na Ollie Watkins kuwa washambulizi ambao wataiwakilisha Uingereza.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 pia alichagua viungo Trent Alexander-Arnold, Conor Gallagher, Curtis Jones, Kobbie Mainoo, Declan Rice na Adam Wharton kwenye kikosi.

Katika safu ya ulinzi, aliwachagua Jarrad Branthwaite, Lewis Dunk, Joe Gomez, Marc Guehi, Ezri Konsa, Harry Maguire, Jarrel Quansah, Luke Shaw, John Stones, Kieran Trippier, na Kyle Walker.

Dean Henderson, Jordan Pickford, Aaron Ramsdale, na James Trafford ndio makipa waliojumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 33.

Kikosi hicho hata hivyo kitapunguzwa hadi wachezaji 25 kabla ya kuanza kwa Euro 2024 mnamo Juni.

Wakati akijibu kuhusu orodha ya wachezaji waliochaguliwa, Rashford ambaye amekuwa akiiwakilisha nchi yake tangu 2016 hakuonyesha hisia mbaya na aliitakia timu kila la heri.

"Namtakia Gareth na vijana kila la heri katika mchuano ujao," Rashford alisema kupitia Instagram.

Aliambatanisha taarifa yake na picha ya orodha ya wachezaji waliochaguliwa kwa Euro.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved