Cristiano Ronaldo alivunja rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja ndani ya ligi ya Saudia baada ya kufikisha magoli 35.
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United alifunga bao la kuongoza kipindi cha kwanza na tena dakika ya 69 kwa kichwa huku Al Nassr ikiilaza Al Ittihad 4-2 nyumbani siku ya Jumatatu.
Rekodi ya hapo awali ya mabao mengi ndani ya msimu mmoja ilikuwa 34 iliyofungwa na Mmorocco Abderrazak Hamdallah mnamo 2018-19.
Ronaldo amefunga mabao 64 katika michezo 69 akiwa na Al-Nassr katika michuano yote tangu ajiunge nayo kwa uhamisho wa bila malipo Januari 2023 baada ya kuondoka Manchester United. Ushindi huo ulimaanisha Al-Nassr kumaliza nafasi ya pili kwenye jedwali kwa msimu wa pili mfululizo, pointi 14 nyuma ya mabingwa Al-Hilal lakini 17 mbele ya Al-Ahli walio nambari tatu.
Ronaldo, ambaye aliiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa michuano ya Euro 2016, amechaguliwa kwenye kikosi kitakachoshiriki makala ya mwaka huu nchini Ujerumani mwezi ujao - michuano yake ya 11 ya kimataifa.
Nyota huyo anasalia kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika soka la kimataifa la wanaume akiwa na mechi 206 na amefunga mabao 128.