Kitengo cha uadilifu katika riadha kimempiga Josephine Chepkoech marufuku ya miaka saba baada ya kutumia dawa iliyopigwa marufuku.
Matokeo ya Chepkoech kuanzia Februari 18 mwaka huu pia yamefutiliwa mbali. Bingwa huyo wa Geneva Marathon 2019 alisimamishwa kwa muda na kitengo cha uadilifu cha riadha mnamo Mei 9, 2024.
Chepkoech alipewa notisi ya madai ya kukiuka Kifungu cha 2.1 na Kifungu cha 2.2 cha kanuni za masharti za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli.
Kitengo hicho kilieleza kuwa mnamo Februari 18, Chepkoech alitoa sampuli ya mkojo wakati wa mashindano yake katika mbio za Seville Marathon ambapo alimaliza wa pili katika mbio hizo na baada ya mkojo wake kupimwa, ikabainika kuwa na dawa zilizopigwa marufuku.
Kitengo hicho kilitoa chapisho kupitia ukurasa wa X iliyodokeza;
"AIU imempiga marufuku Josephine Chepkoech (Kenya) kwa miaka 7 kuanzia tarehe 7 Mei 2024, kwa Kuwepo/Matumizi ya Dawa Iliyokatazwa (Testosterone). Matokeo ya DQ kutoka 18 Februari 2024."
Ilibainika zaidi kuwa mwanariadha huyo hakusamehewa kwa matumizi ya dawa hiyo maarufu. Mwanariadha huyo alikubali uamuzi huo lakini hii ilikuwa mara yake ya pili kujikuta katika upande mbaya wa sheria, baada ya kukiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli.
Hapo awali alikuwa ametumikia kipindi cha kutostahiki kwa miaka miwili kutoka 2015 hadi 2017. Mwanariadha huyo alitakiwa kutumikia marufuku ya miaka minane lakini baada ya kukubali uamuzi huo na kujibu kwa wakati, atatumikia marufuku hiyo kwa miaka saba.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 35 alishiriki kwa mara ya kwanza katika mbio za marathon mwaka wa 2018 katika mbio za Nairobi Marathon, ambapo alitawala saa 2:33:11.