Nahodha wa Argentina,Lionel Messi ameelezea furaha yake baada ya timu yake kufika kwenye fainali ya kombe la Copa America 2024 baada ya kuiadhibu Canada 2-0.
Messi alifunga bao lake la kwanza la michuano hiyo katika dakika ya 51 na kuisaidia Argentina kuwa na bao la pili baada ya Julian Alvarez kupachika la kwanza. Kufuatia ushindi huo, Messi mwenye furaha alisema anafurahia ‘vita vyake vya mwisho’ na taifa hilo la Argentina.
“Si rahisi kuwa kwenye fainali nyingine, kushindana tena ili kuwa mabingwa, tunachokipata ni kigumu sana na tunatakiwa kutumia fursa hiyo. Si rahisi kufanya hivi na tunafanya tena," Messi alisema.
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake , alisema kuwa;
“Ninajua, kama ilivyo kwa Otamendi, Di María na mimi, kwamba hizi ni vita vya mwisho na tunavifurahia kwa ukamilifu.”
Ushindi huo wa Argentina umewapa fursa nyingine ya kuhakikisha kuwa wanatetea taji hilo la Copa America baada ya kuishinda Brazil 1-0 mwaka wa 2021.
Argentina sasa itashiriki katika mpambano wa kilele huko Miami Jumapili ambapo watamenyana na mshindi kati ya Colombia na Uruguay mechi ambayo imeratibiwa kuchezwa Alhamisi,Julai 11 2024.