Klabu ya soka ya Arsenal imetangaza kuondoka kwa wachezaji wawili, kiungo wa kati Albert Sambi Lokonga na beki wa kushoto Nuno Tavares.
Klabu hiyo yenye maskani yake London ilithibitisha Jumatatu kwamba wachezaji hao wawili waliojiunga nao mwaka wa 2021 wameondoka klabu hiyo kwa mkopo.
Lokonga amejiiunga na klabu ya Sevilla ya Uhispania kwa mkopo wa msimu mzima huku klabu hiyo ya Laliga ikiwa chaguo la kumnunua kwa euro milioni 12.
"Hatua hii inayofuata katika taaluma ya Sambi inawakilisha fursa nzuri kwa kiungo wetu wa kimataifa wa Ubelgiji kutimiza uwezo wake zaidi kwa kushindana kwa kiwango cha juu katika ligi kuu ya Uropa. Kila mtu katika Arsenal anamtakia kila la kheri Sambi msimu huu ujao akiwa na Sevilla. Mkataba wa mkopo unategemea kukamilika kwa michakato ya udhibiti," Arsenal FC ilisema katika taarifa.
Inaripotiwa kuwa mshahara kamili wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24 utalipwa na Sevilla FC.
Kwa upande wa beki Nuno Tavares, aliachiliwa kujiunga na klabu ya Italia Lazio Roma kwa mkopo wa msimu mzima.
Arsenal ilisema kuwa dili hilo la beki mwenye umri wa miaka 24 linategemea kukamilika kwa taratibu za udhibiti.
"Hatua hii katika maisha ya Nuno ni fursa nzuri ya kujiendeleza zaidi kwa kupata uzoefu muhimu katika Serie A na kandanda ya Italia. Kila mtu Arsenal anamtakia Nuno kila la heri msimu huu ujao akiwa na Lazio. Mkataba wa mkopo unategemea kukamilika kwa michakato ya udhibiti," Arsenal ilisema.
Inaripotiwa kuwa Lazio imetakiwa kumnunua mchezaji huyo wa Ureno baada ya kumalizika kwa muda wa mkopo.