Chelsea "imeanzisha utaratibu wa ndani wa nidhamu" kufuatia video ya Enzo Fernandez iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo Shirikisho la Soka la Ufaransa linadai kuwa ni la ubaguzi wa rangi.
Fernandez na baadhi ya wachezaji wenzake wa Argentina walikuwa wakiimba wimbo wa dharau kuhusu timu ya Ufaransa katika video ya moja kwa moja ya Instagram iliyochapishwa kwenye akaunti yake baada ya kuifunga Colombia katika fainali ya Copa America siku ya Jumapili.
Wesley Fofana, mchezaji mwenza wa Fernandez wa Chelsea, alichapisha tena video hiyo kwenye X na maneno haya: "Soka mwaka 2024: ubaguzi wa rangi usiozuiliwa".
Fernandez baadaye aliomba msamaha kwenye Instagram kwa kuchapisha video hiyo na kosa lolote ambalo maudhui yake yanaweza kusababisha
Jumatano asubuhi Chelsea ilitoa taarifa ya klabu:
“Klabu ya Soka ya Chelsea inaona aina zote za tabia za kibaguzi hazikubaliki kabisa. Tunajivunia kuwa klabu kubwa inayojumuisha watu wote ambapo watu kutoka tamaduni zote, jumuiya na utambulisho hujisikia wamekaribishwa.
Tunakubali na kuthamini msamaha wa hadharani wa mchezaji wetu na tutatumia hii kama fursa ya kuelimisha.
Klabu imeanzisha utaratibu wa ndani wa nidhamu.”
Kauli ya The Blues inakuja baada ya Fernandez kusema "samahani sana" kwa video hiyo.
"Wimbo huu una lugha ya kuudhi sana na hakuna kisingizio kabisa cha maneno haya," kijana huyo wa miaka 23 alisema.
"Ninapinga ubaguzi wa aina zote na ninaomba radhi kwa kushikwa na shangwe za sherehe zetu za Copa America. Video hiyo, wakati huo, maneno hayo, hayaakisi imani yangu au tabia yangu. Samahani kweli."