Klabu ya Chelsea imetoa orodha rasmi ya wachezaji wake watakaoshiriki msururu wa mechi za kujifua kwa ajili ya msimu mpya nchini Marekani.
Klabu hiyo, kama vilabu vingine vingi tu vinatarajiwa kusafiri kuelekea Marekani kwa ajili ya mechi za kujiandaa kwa ajili ya msimu mpya zitakazoanza wikendi hii.
Katika orodha ya wachezaji ambao wanasafiri, Chelsea imewaacha nje baadhi ya wachezaji tajika katika kikosi cha msimu jana kilichomaliza katika nafasi ya 6 kwenye msimamo wa jedwali la ligi kuu, EPL.
Mfungaji bora wa klabu hiyo msimu jana Cole Palmer ni mmoja wa majina makubwa ambayo hayamo kwenye orodha hiyo huku Conor Gallagher ambaye alicheza kama nahodha katika baadhi ya mechi msimu jana pia akikosekana kwenye orodha hiyo ya wachezaji 28.
Mlinda lango Djodje Petrovic ambaye alitumika sana baada ya kuumia kwa Robert Sanchez pia hayuko kwenye orodha hiyo, Moises Caicedo, Enzo Fernandez pamoja na beki mshindi wa Euro 2024 na Uhispania, Marc Cucurella.
Hata hivyo, sajili mpya Marc Guiu, Kernan Dewsbury-Hall, Tosin Adarabioyo, Renato Veiga wote wamejumuishwa kwenye kikosi.
Hii hapa orodha kamili ya wachezaji 28 watakaosafiri kwenda Marekani;
Makipa: Sanchez, Bettinelli, Beach, Bergstrom
Mabeki: James, Gusto, Acheampong, W Fofana, Disasi, Tosin, Badiashile, Colwill, Chilwell, Veiga
Viungo: Chukwuemeka, Lavia, Ugochukwu, Dewsbury-Hall, Santos
Washambuliaji: Jackson, Nkunku, Sterling, Mudryk, Madueke, Broja, George, Guiu, Angelo.