logo

NOW ON AIR

Listen in Live

‘Mashabiki wa Arsenal walinihukumu kwa bei, sio uwezo wangu wa mpira' - Nicholas Pepe

"Kama Arsenal wangeninunua kwa pauni milioni 20, labda ingekuwa tofauti," anasema.

image
na Samuel Maina

Michezo26 July 2024 - 10:08

Muhtasari


  • •"Nilipojiunga kwa mara ya kwanza, mashabiki hawakuwa wakihukumu uchezaji wangu, walikuwa wakipima bei," alisema.
  • •"Kama Arsenal wangeninunua kwa pauni milioni 20, labda ingekuwa tofauti," anasema. "

Nicolas Pepe anakubali kuondoka kwake Arsenal na bei ambayo ilizusha maoni kuhusu uchezaji wake, anakiri "haikuwa rahisi".

Watu wanapomtaja mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 29, pauni milioni 72 zilizoweka rekodi ya klabu wakati huo kumsajili winga huyo kutoka Lille inafuatia.

"Haikuwa rahisi hata kidogo. Na mashabiki hawakufurahishwa na jinsi nilivyokuwa nikicheza," aliambia BBC Sport.

"Nilipojiunga kwa mara ya kwanza, mashabiki hawakuwa wakihukumu uchezaji wangu, walikuwa wakipima bei.. Lakini nadhani nilifanya mambo makubwa nikiwa Arsenal. Sijutii kuchezea Arsenal.

"Lakini ada yangu ya uhamisho kwa klabu ilikuwa ya juu, kwa hivyo walitarajia nifunge katika kila mechi."

Arsenal ilimsajili Pepe 2019 baada ya msimu mzuri na Lille, ambapo alifunga mabao 23 na pasi za mwisho 12, lakini hakuwahi kuwa na kiwango kama hicho huko England.

Aliichezea Arsenal mechi yake ya mwisho mwaka 2022 na, baada ya kuwepo kwa mkopo wa muda mrefu huko Nice, sasa hana klabu baada ya kuondoka Trabzonspor ya Uturuki msimu uliopota, baada ya kujiunga nao kwa uhamisho wa bure kutoka Arsenal Septemba iliyopita.

'Kama Arsenal wangeninunua kwa £20m labda ingekuwa tofauti'

Ilikuwa ndoto ya utotoni ya Pepe kujiunga na Arsenal baada ya kuzawadiwa jezi ya Thierry Henry na kaka yake.

Aliweza kufunga mabao 24 na kutoa pasi za mabao 15 katika mechi 91 katika misimu yake miwili ya kwanza katika soka la Uingereza, anaamini anatazamwa kama alishindwa kwa sababu tu ya ada ya 2019.

"Kama Arsenal wangeninunua kwa pauni milioni 20, labda ingekuwa tofauti," anasema. "Sio kosa la mchezaji.”

"Hawaombi pauni milioni 100 au 90. Lakini ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa soka na ni kitu ambacho watu hawawezi kuelewa.

"Pia kuna wachezaji kama [Mykhailo] Mudryk na Antony ambao hawafanyi vizuri kila wakati, lakini bado si wachezaji wabaya."

'Arteta hakuwa na imani na mimi'

Maelezo ya picha,Kocha wa Arsenal Mikel Arteta na Nicholas Pepe

Licha ya wakati wake mgumu katika Uwanja wa Emirates, Pepe anasema anashukuru jinsi kuondoka kwake 2023 kulivyoshughulikiwa na Arsenal na kwamba bado "anamheshimu" meneja Mikel Arteta.

“Walinisaidia wakati wa kuondoka, jambo ambalo halikuwa rahisi kwa sababu nilikuwa na jeraha , hivyo kupona kwangu haikuwa rahisi... walinisaidia kupata klabu haraka,” alieleza. "Kwa hivyo, hakika niliiacha klabu kwa makubaliano mazuri.

"Siku zote nimekuwa na uhusiano mzuri na Arteta. Ni kwamba tu hakuwa na imani na mimi, ambayo ni aibu.

"Aliweka pamoja timu nzuri, na cha kusikitisha, sikuwa katika mabadiliko hayo ya wachezaji. Lakini ni mtu ninayemheshimu, na najua ananiheshimu pia. Na ninamtakia kila la heri."

Pepe sasa anahisi wakati mgumu utamfanya kuwa na nguvu kiakili.

"Kwa shinikizo nililopitia Arsenal, niko kwenye nafasi nzuri sasa," alisema.

"Ni kitu ambacho sizingatii tena kwa sababu unapopata ukosoaji mwingi, unakuwa sugu . Kwa hivyo, sasa niko tayari kwa tukio lolote. Ninahisi kama niko kwenye nafasi nzuri."

'Sitaondoa uwezekano wa kurudi England'

"Imepita miaka miwili tangu nifanye maandalizi ya msimu mpya. Na ninajisikia vizuri ninapoanza mechi za maandilizi ya kufungua msimu. Niko katika hali nzuri kiafya, nahitaji kurejea kuwa mchezaji mwenye kasi niliyekuwa zamani."

Pepe alionekana katika hali ya matumaini baada ya mkutano kati yake na wakala wake kuhusu hatua yake inayofuata. Anatumai kuwa hivi karibuni ataweza kutoa habari kuhusu klabu yake ijayo na hashangai kurejea kwenye soka la Uingereza ili kuwakabili wakosoaji hao.

"Hakika nilijifunza mengi," alisema. "Ndio, bila shaka, mimi ni mchezaji yule yule. Ninazeeka, ambayo ni kawaida, lakini bado ni mchezaji yule yule.

"Kwa hakika ninaweza kuiga uchezaji wangu wa zamani. Ninahitaji tu kucheza kulingana na hali yangu ya kimwili, imani ya klabu na upendo kutoka kwa mashabiki. Kwa hiyo, inahusisha yote hayo.

"Tunapoona mchezaji akicheza vizuri na kufunga mabao mengi, ni kwa sababu ana vitu hivyo vyote karibu naye: kocha anayemsaidia, klabu, na mashabiki wanaopenda. Kwa hivyo, nadhani hiyo ni muhimu kwa mchezaji kucheza vizuri."

Aliongeza: "Tunasikiliza ofa zote, halafu ni wawakilishi wangu ambao watanijulisha nia ya kweli ya klabu, na ikiwa sio ofa nzito, siisikii. Wacha tuone nini kitatokea. Lakini mimi" Sitaondoa uwezekano wa kurudi Uingereza."


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved