Waandalizi wa Olimpiki nchini Ufaransa walicheza wimbo wa taifa usio sahihi kwa Sudan Kusini kabla ya mchezo wa ufunguzi wa mpira wa vikapu wa wanaume dhidi ya Puerto Rico.
Mashabiki katika uwanja wa Pierre Mauroy siku ya Jumapili walilalamika huku wimbo wa Sudan ukipigwa badala ya ule wa Sudan Kusini.
Sauti ilirekebishwa baada ya kusitishwa kwa muda mfupi, na kufuatiwa na shangwe kutoka kwa umati.
Waandalizi wa Michezo ya Olimpiki huko Paris walitoa taarifa wakiomba msamaha kwa "kosa la kibinadamu".
Mmoja wa wachezaji wa Sudan Kusini baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa mhusika "hakuheshimu".
"Wao [waandaji] wanapaswa kuwa makini zaidi kwa sababu hii ndiyo hatua muhimu zaidi, na unajua kwamba Sudan Kusini inacheza," alisema Majok Deng.
"Hakuna namnaa unaweza kukosea kwa kucheza wimbo tofauti. Ni kukosa heshima," aliendelea.
"Ni wazi, hakuna mtu mkamilifu. Walifanya makosa. Waliirekebisha mwishoni, na tukaendelea."
Waandalizi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 waliomba "radhi zao za dhati kwa timu ya Sudan Kusini na mashabiki wao kwa makosa hayo."
"Tunaelewa uzito wa makosa," ilisoma taarifa hiyo.
Ni mara ya pili kwa waandaaji kuomba radhi kwa kosa kama hilo - wakati wa sherehe za ufunguzi siku ya Ijumaa, wanariadha wa Korea Kusini walitambulishwa kimakosa kama "Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea" - jina rasmi la Korea Kaskazini.