Bingwa wa mbio za marathon, Eliud Kipchoge kutoka Kenya, amekosa nafasi ya kuwa mwanariadha wa kwanza katika historia kushinda medali tatu za dhahabu za marathoni katika mashindano hayo.
Bingwa huyo wa marathon hakuweza kuendana na kasi ya washindani wake katika nusu ya safari wakati wa mbio za marathon za Olimpiki ya Paris Jumamosi asubuhi, na kuua ndoto yake ya kuwa bingwa kwa mara ya tatu mfululizo. Alishikilia nafasi ya 63 baada ya kukimbia kwa kilomita 25 ya mbio hizo za 42km.
Tamirat Tola wa Ethiopia alifika ukingoni baada ya saa 2:06.26, na kuvunja rekodi ya Olimpiki na pia kupata dhahabu ya kwanza ya nchi yake katika michezo hiyo.
Mwanariadha wa Ubelgiji Bashit Abdi (2.06.47) alimaliza wa pili na kutwaa medali ya fedha, huku Mkenya Benson Kipruto akishinda shaba kwa kutumia saa 2:07:00.
Kipchoge alikuwa anatazamia kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda mataji matatu ya marathon katika michezo hiyo.
Kando na kuwa katika uwanja unaotawaliwa na washindani wadogo, Kipchoge pia alikuwa akipambana na hali ya hewa na milima.
"Barabara ni ngumu - karibu asilimia 40 ni ya vilima - na nadhani hali ya joto itachangia sana," aliiambia BBC Sport Africa awali.
"Hata saa mbili, tatu, nne asubuhi, nadhani itapanda hadi digrii 30. Ni ngumu kukimbia marathon kamili (katika) digrii 30.
"Itatuchukua muda mwingi kwetu kupata hali ya hewa, kuandaa akili kupitia hali ya joto kali kwenye kozi."
Mwezi Aprili, Kipchoge alisema "matarajio yake makubwa" yalikuwa kushinda mjini Paris licha ya kumaliza nambari 10 kwenye mbio za Tokyo Marathon za Machi - nafasi yake ya chini kabisa ya ushindani kuwahi kutokea.
"Nitaweka shinikizo zaidi [kwenye] na matarajio mengi yapo," alisema.
"Ikiwa nitapoteza marathon basi nitakatishwa tamaa. Lakini basi narudi na kuanza safari tena.”