Licha ya kuondoka PSG zaidi ya miezi miwili iliyopita, Kylian Mbappe bado yuko kwenye mzozo na wamiliki wa klabu hiyo, Qatar Sports Investments, jambo ambalo linaweza kuwagharimu mabingwa wa Ufaransa nafasi yao kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Kulingana na Le Monde, Mbappe bado hajapokea Euro milioni 55 (Sh7.86bn) ambazo anadai anadaiwa kutokana na mkataba wake wa mwisho na PSG.
Hii ni pamoja na awamu ya mwisho ya bonasi yake ya kusaini yenye thamani ya Euro milioni 36 (£30.6m), ambayo ilipaswa kulipwa mwezi Februari, pamoja na miezi mitatu ya mwisho ya mshahara wake kutoka kwa mkataba wake wa Aprili, Mei na Juni.
Mbappe anadai pia anastahili kulipwa 'bonasi ya kimaadili' kwa miezi hii mitatu aliyokosa, huku wakili wa mchezaji huyo akiitumia PSG notisi rasmi katikati mwa Juni, kama ilivyofichuliwa na L'Equipe.
Ripoti hiyo inadai kuwa licha ya kujaribu kuepusha mzozo mkubwa, kuendelea kwa Mbappe kushindwa kupata malipo kumemlazimu kijana huyo mwenye umri wa miaka 25 kuchukua hatua kali.
Sasa ameripotiwa kupeleka suala hilo kwa kamati ya sheria ya Ligi ya Soka ya Wataalamu wa Ufaransa (LFP) na, kupitia Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF), kwa shirikisho la soka la Ulaya, UEFA.
Kuhusika kwa LFP kunaweza kuishia kuwa mbaya kwa PSG kwani shirika hilo lina uwezo wa kutekeleza marufuku ya uhamisho kwa klabu hiyo, pamoja na kuwanyima leseni ya UEFA - jambo ambalo lingesababisha kufungiwa mara moja kutoka kwa Ligi ya Mabingwa.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa klabu yoyote inayoshiriki katika mashindano ya UEFA lazima itoe uthibitisho kuwa haina malipo ambayo hayajalipwa kwa wafanyikazi wao kabla ya Februari 28 kabla ya msimu wa leseni.
Kwa hivyo, PSG wako katika hatari ya kupoteza leseni ya klabu ya UEFA iliyotolewa kwa kampeni ya 2024/25 ikiwa suala na Mbappe halitatatuliwa.
Kama ilivyoripotiwa na Get French Football News, PSG wanadai kuwa kushikiliwa kwa malimbikizo ya mishahara ya Mbappe yanahalalishwa na 'ahadi' alizotoa mchezaji huyo kuzikataa endapo ataondoka kama mchezaji huru.
Walakini, inadaiwa kuwa 'hakuna makubaliano ambayo yameidhinishwa kati ya pande hizo mbili tangu 2023 kuhusu suala hilo'.