Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes amekiri kuwa aliomba msamaha kwa meneja wa zamani wa Manchester United Erik ten Hag baada ya kutimuliwa wiki iliyopita.
Ten Hag alifukuzwa na United Jumatatu iliyopita baada ya kusimamia ushindi mara tatu pekee kutoka kwa mechi tisa za ufunguzi za Ligi Kuu msimu huu.
United walifanya haraka kuteua mrithi wa Mholanzi huyo, na kumgeukia bosi wa Sporting Lisbon Ruben Amorim, ambaye ataanza rasmi kazi Old Trafford mnamo Novemba 11.
Hadi Amorim anawasili Uingereza, Ruud van Nistelrooy ndiye anayeshikilia ngome, na alisimamia sare ya 1-1 na Chelsea kwenye Uwanja wa Old Trafford Jumapili, ikimaanisha kuwa ameshinda moja na kutoka sare moja kati ya michezo yake miwili ya ufunguzi akiwa meneja wa muda.
United walidhani wangepata ushindi unaohitajika sana wa Ligi ya Premia baada ya Fernandes kuwafungia bao la kuongoza baada ya dakika 70, kwa njia ya mkwaju wa penalti, na Moises Caicedo akaisaidia Chelsea dakika nne baadaye kwa bao zuri.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza tangu Ten Hag aondoke kwenye klabu hiyo, Fernandes alifichua kuwa aliomba msamaha kwa meneja huyo wa zamani baada ya klabu hiyo kufanya uamuzi wa kumfukuza kazi, akikiri alihisi kana kwamba alichangia uamuzi huo.
"Tunajua kwamba Erik ameondoka, si vizuri kwa yeyote katika klabu wakati meneja anapokwenda," Fernandes alikiri, akizungumza na Sky Sports.
“Timu ikiwa si bora, matokeo si bora ni yeye [Ten Hag] ndiye anayelipa. Kila unapoona meneja anaenda lazima ujilaumu mwenyewe, ni kwa sababu timu haifanyi vizuri, ni rahisi kumuondoa meneja kuliko wachezaji 15.”
"Nilizungumza na meneja [Ten Hag] na kumuomba msamaha, nilikata tamaa kwamba ameenda na nilijaribu kumsaidia. Sikuwa nikifunga mabao, hatufungi mabao na ninajisikia kuwajibika. Kwa kawaida huwa nafunga mabao mengi lakini kila mara nilitoa asilimia 100. Anafahamu hilo."