TIMU ya taifa ya Kenya
kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 20 wanatarajiwa kuchuana na timu ya
Tottenham ya UIngereza ya vijana wasiozidi umri wa miaka 23 katika mechi mbili
za kirafiki.
Haya ni kwa mujibu wa
naibu Kamishna Mkuu wa Kenya katika jimbo la St. James mjini London, Joseph
Warui.
Warui alitangaza mipango
ya kuandaa mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Kenya U20 na Tottenham
Hotspur U23 ambayo itachezwa kwa mikondo miwili, moja nchini Uingereza na
nyingine Uturuki.
Warui alitangaza hayo
baada ya kukutana na nahodha wa zamani wa Harambee Stars Victor Wanyama jijini
London siku ya Jumatatu.
Wawili hao walijadili
mada mbalimbali, ikiwemo uwezekano wa Kenya kucheza na Tottenham nchini
Uingereza na Asia.
Hata hivyo,
hakuthibitisha iwapo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilihusika katika
majadiliano hayo.
Wanyama ambaye ni kiungo
wa zamani wa Tottenham Hotspur, aliyekaa miaka minne katika klabu hiyo ya
Kaskazini mwa London alikuwa muhimu katika kuongoza mijadala ya kuandaa mechi
ya maonyesho.
"Tunaandaa mechi ya
kirafiki mnamo Desemba kati ya Timu ya Taifa ya U20 ya Kenya na Tottenham
Hotspur U23 nchini Uturuki na Uingereza," Warui
alisema katika taarifa.
Mechi hii ya kirafiki
itakuwa ya manufaa kwa timu ya Kenya ya U20 inapojiandaa kwa Kombe la Mataifa
ya Afrika U20 (AFCON) mwaka ujao, ambayo pia itatumika kama kufuzu kwa Kombe la
Dunia la U20 nchini Chile.
Huku timu ya wakubwa
Harambee Stars ikiwa inasuasua hadi kubanduliwa nje ya mashindano ya AFCON
mwakani nchini Morocco, vijana wa Rising Stars na kina dada wasiozidi umri wa
miaka 17 wa Harambee Starlets wamesalia kuwa wa pekee kuipeperusha bendera ya
Kenya katika mashindano ya kimataifa.
Itakumbukwa Rising Stars
walitinga kwenye fainali ya CECAFA ambapo walichapwa mabao 2-1 na Tanzania.
Kwa upande mwingine,
wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 walikuwa timu ya taifa ya kwanza kutoka
Kenya kufuzu katika mashindano ya kombe la dunia.
Mashindano hayo
yalifanyika katika jamhuri ya Dominika ambapo wasichana hao walishinda mechi
moja tu kwenye kundi lao dhidi ya Mexico.