logo

NOW ON AIR

Listen in Live

FKF yaahidi kuajiri kocha stadi kuiongoza Harambee Stars

Hili linajiri baada ya kocha mkuu wa Harambee Stars Engin Firat kujiuzulu.

image
na Tony Mballa

Michezo12 December 2024 - 08:37

Muhtasari


  •  Kujiuzulu kwa Firat kunakuja siku moja tu baada ya Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen kusema kuwa serikali haitamlipa tena mshahara wa wake na kuitaka ofisi mpya ya FKF kumtimua.
  • Kulingana na Murkomen, kandarasi ya Firat ilimtaka ajiuzulu ikiwa Kenya haitafuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 nchini Morocco, hitaji ambalo Firat sasa ameshindwa kutimiza.

 




Shirikisho la soka nchini Kenya limeahidi kuajiri kocha stadi ambaye ataisaidia timu ya taifa Harambee Stars kusajili matokeo mazuri.

Hili linajiri baada ya kocha mkuu wa Harambee Stars Engin Firat kujiuzulu na kutamatisha miaka yake mitatu yenye msururu wa matatizo.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya Hussein Mohammed alithibitisha hilo wakati wa kikao na wanahabari katika Jumba la Kandanda jijini Nairobi siku ya Jumatano, na kuongeza kuwa shughuli ya kutafuta kocha mpya inaendelea.

Pembeni yake alikuwa naibu wake McDonald Mariga na Mkurugenzi Mtendaji wa FKF Patrick Korir.

"Tumepokea mawasiliano ya kocha mkuu wa timu ya taifa Engin Firat. Suala hilo limefikishwa katika ofisi mpya kwa ajili ya kujadiliwa," Hussein alisema.

“Kama mnavyofahamu, Kenya pamoja na Uganda na Tanzania watakuwa wenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani, na kama shirikisho tunatakiwa kusonga mbele kwa kasi ili kuanza maandalizi mapema,” alisema Hussein.

Hussein alisema shirikisho hilo litashirikisha washikadau ili kuhakikisha Kenya inaajiri mtu anayefaa ambaye anaweza kuandikisha matokeo mazuri. Hata hivyo, haikubainika iwapo wananuia kuajiri kocha wa kigeni au mzaliwa wa Kenya.

"FKF itaenda kwa kasi kushughulikia suala lililopo na kutoa mwelekeo kwa wakati ufaao," Hussein alisema.

Hussein alisema timu ya taifa itaitwa kupiga kambi hivi karibuni ili kuanza kunoa makali kwa ajili ya mashindano ya Chan Februari.

Kujiuzulu kwa Firat kunakuja siku moja tu baada ya Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen kusema kuwa serikali haitamlipa tena mshahara wa wake na kuitaka ofisi mpya ya FKF kumtimua.

Kulingana na Murkomen, kandarasi ya Firat ilimtaka ajiuzulu ikiwa Kenya haitafuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 nchini Morocco, hitaji ambalo Firat sasa ameshindwa kutimiza.

Murkomen alikuwa ameelezea kutoridhishwa kwake na utendakazi wa Firat, akibainisha rekodi mbaya ya kocha huyo ya kushinda mara tatu tangu kuwasili kwake miaka mitatu iliyopita.

“Nimeona kandarasi ya kocha wa Harambee Stars, na inadhihirisha wazi kwamba anafaa kuondoka ikiwa hatafuzu kwa AFCON.

"Iwapo FKF inataka kumbakiza, italazimika kumlipa mshahara wake kutoka kwa pesa zao wenyewe kwa sababu hakutimiza masharti ya kandarasi," Murkomen alisema kwenye mahojiano.

Murkomen alikiri kwamba ingawa wengi walikuwa wametoa wito wa kufutwa kazi kwa Firat, mamlaka ya kumwajiri au kumfuta kazi kocha huyo ni ya FKF pekee.

"Kumekuwa na wito mwingi wa kufutwa kazi kwa Firat, lakini FKF ina mamlaka ya kipekee ya kufanya uamuzi huo. Hatuwezi kuingilia kati,” alisema.

Alikosoa uamuzi wa kuajiri Firat, akibainisha kuwa gaffer wa Kituruki hakuwa na hadithi ya mafanikio.

“Sijui Nick Mwendwa alitumia vigezo gani kumwajiri. Hakuwa na rekodi ya kuvutia. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba mshahara wake hulipwa na walipa ushuru, jambo ambalo si la kawaida kwa sababu hakuna kocha mwingine anayelipwa na serikali,” Murkomen aliongeza.

Katika mahojiano ya awali na vyombo vya habari vya ndani, Firat alithibitisha kuwa amekubali kujiuzulu.

"Niliruhusu Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutangaza, lakini nimekatisha kandarasi yangu baada ya Waziri kuzungumza mengi kunihusu," Firat alisema.

Mchezo wa mwisho wa Firat kama mkufunzi wa Harambee Stars ulikuwa sare ya 0-0 dhidi ya Namibia mwezi uliopita.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved