logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kuwa Kocha Wa Mpira Ni Kazi Ngumu Kuliko Kuwa Mwanasiasa – Kocha Wa Tottenham

Alipoulizwa kama usimamizi ulikuwa mgumu kuliko kuwa waziri mkuu, raia huyo wa Australia mwenye umri wa miaka 59 aliongeza: "Ah ndio, ana uchaguzi mara ngapi? Nina uchaguzi kila wikendi.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Michezo20 December 2024 - 11:35

Muhtasari


  • Spurs, ambao hawajashinda kombe lolote tangu 2008, wanaendelea na kampeni yao ya Kombe la Carabao baada ya kuititiga Manchester United
  • Postecoglou anasema kumaliza ukame wa vikombe vya klabu kunaweza kusaidia kubadilisha hali ya mashabiki. 



KOCHA wa Tottenham Hotspur Ange Postecoglou anasema usimamizi wa soka ndio "kazi ngumu zaidi katika nyanja yoyote ya maisha" - ikiwa ni pamoja na kuwa waziri mkuu.


Postecoglou, ambaye timu yake ilimaliza msururu wa michezo mitano bila kushinda katika ushindi wa Jumapili wa Ligi Kuu dhidi ya klabu ya Southampton, anasema anakabiliwa na kazi ngumu "kila wikendi".


Ushindi huko St Mary's uliwapa Spurs hadi nafasi ya 10 kwenye jedwali lakini ukamgharimu meneja wa Saints Russell Martin, saa chache baada ya klabu nyingine inayoshiriki ligi kuu ya Wolves kuachana na kocha Gary O'Neil.


"Kazi hii ndiyo kazi ngumu zaidi sasa katika nyanja yoyote ya maisha. Unaweza kusema siasa, lakini hii ni ngumu kuliko kazi yoyote," alisema Postecoglou Jumatano.


"Muda na maisha marefu ya jukumu hili sasa inamaanisha kwamba unaingia ndani yake na wachache sana watatoka bila makovu yoyote."


Postecoglou amekabiliwa na ukosoaji wa timu yake kutokuwa na msimamo katika wiki za hivi karibuni na akachagua kukabiliana na wafuasi waliochukizwa baada ya kushindwa na Bournemouth mwezi huu.


Alipoulizwa kama usimamizi ulikuwa mgumu kuliko kuwa waziri mkuu, raia huyo wa Australia mwenye umri wa miaka 59 aliongeza: "Ah ndio, ana uchaguzi mara ngapi? Nina uchaguzi kila wikendi.


"Tuna uchaguzi kila wikendi na tunapigiwa kura ndani au nje.”


"Tumepoteza aina zote za heshima katika jamii yetu ambapo wavulana wako kazini na wanaweka majina ya nani atakayechukua nafasi zao wakati bado wanafanya kazi.”


"Kama jamii, tuna haraka sana kutupa watu kwenye takataka na kusonga mbele kwa haraka bila mawazo wala kujali. Sijui kama kuna njia nzuri au njia bora ya kulishughulikia."


Spurs, ambao hawajashinda kombe lolote tangu 2008, wanaendelea na kampeni yao ya Kombe la Carabao baada ya kuititiga Manchester United kibano cha mabao 4-3 usiku wa Alhamisi.


Postecoglou anasema kumaliza ukame wa vikombe vya klabu kunaweza kusaidia kubadilisha hali ya mashabiki.


"Ikiwa nitaendelea na maoni ya jumla tangu nimekuwa kwenye kazi hii, ninahisi kama kombe litafanya mahali hapa kubadilika kuwa kitu, kwa hivyo wacha tuone," alisema.


"Mimi binafsi? Kama ninavyoendelea kusema, nataka zaidi ya hivyo. Sidhani kama ni kupata kombe tu.”


“Nafikiri unapotaka kujenga klabu yenye mafanikio na endelevu katika kuwania mataji kila mwaka, ni zaidi ya hapo, lakini haitakuwa mara ya kwanza kukosea kitu nikiwa kwenye kazi hii. Labda kombe ndilo linalohitaji, sijui."



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved