Kocha wa Fenerbahce Jose Mourinho amewahakikishia mashabiki wa soka kuwa hali yake ya afya ni njema baada ya tetesi kuenea mitandaoni kuwa alikuwa mgonjwa.
Akitoa hakikisho hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mourinho amesema kuwa alifanyiwa upasuaji mdogo ila taarifa zilizoenezwa mtandaoni zilikuwa zimetiwa chumvi mno.
Kwa mujibu wa majarida ya spoti ya ughaibuni, ziliripoti kuwa kocha huyo aliyewahi kuzifunza timu za Chelsea, Manchester United na Real Madrid alisafiri baada ya mchuano baina ya Fenerbahce na Eyupspor ulioishia kwa sare ya moja kwa moja ili kufanyiwa upasuaji mdogo katika taifa lingine.
Kocha huyo aliyewatakia sherehe njema za krisimasi kwa wafuasi wake alisema kwamba atarejea kwa mazoezi pindi tu baada ya mapumziko ya sherehe.
“Nawatakia kilammoja msimu wa sherehe wa furaha. Wakati huu ujawe na upendo na furaha kwenu na familia zenu.” Aliandika Mourinho kwenye ujumbe ulioambatana na video kwenye mtandao wa Instagram.
Aidha kwa wale walioonyesha wasiwasi kuhusu hali yake ya afya, kocha huyo ambaye timu yake inashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali aliwahakikishia kuwa hali yake ya siha ni njema kinyume na taarifa zilizotiwa chumvi zilizoenezwa mtandaoni ziliarifu.
“Kwa wale ambao waonyesha wasiwasi, naweza dhibitisha kwamba taarifa za
upasuaji zimetiwa chumvi. Upasuaji huo ni utaratibu wa haraka na mdogo tu.” Alisema Jose Mourinho.
Wakati huo alifichua kwamba hajawai kukosa
kuhudhuria mazoezi katika miaka 25 iliyopita akihakikisha kwamba hataraji
kukosa mazoezi na timu yake kuanzia sasa.