Talanta FC waliwazaba AFC Leopards 4-2 katika uwanja wa Dandora Jumamosi. Ushindi huo uliashiria ushindi wa kwanza wa Talanta wa Ligi Kuu dhidi ya Ingwe katika jaribio lao la saba tangu kupandishwa daraja hadi ligi kuu msimu wa 2021/2022.
AFC Leopards ambao hawakuwa wamepoteza chini ya kocha mkuu Fred Ambani kabla ya mechi hiyo, walitangulia kufunga katika dakika ya 12 kupitia Bonface Munyendo.
Talanta walisawazisha dakika mbili baadaye kupitia kwa Kevin Odongo kabla ya bao la Brian Kipruto kuwaweka kifua mbele katika dakika ya 19.
Hali ilizidi kudorora wakati Emmanuel Osoro alipofunga bao la tatu, dakika chache tu baada ya kurejea kwa mchezo katika kipindi cha pili.
Matumaini ya Leopards kuzoa alama kwenye mechi hiyo yaligonga mwamba baada ya mshambuliaji matata wa Talanta Kipruto kupachika wavuni bao la nne, huku Maxwell Otieno akipatia Leopards bao lao la pili.
Ushindi huo unaipandisha Talanta hadi nafasi ya 15 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya na kutoka kwenye eneo la kushushwa daraja kwa muda.