NAHODHA wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars Michael Olunga ameonyesha furaha yake baada ya klabu yake ya Al Duhail ya nchini Qatar kumsajili aliyekuwa winga wa Chelsea, Hakim Ziyech.
Al Duhail ilitangaza usajili wa
mchezaji huyo wa Morocco ambaye alikatisha mkataba wake na miamba wa Uturuki, Galatassary.
Baada ya kutoa tangazo hilo, Olunga
kupitia ukurasa wake wa X aliandika ujumbe wa kumkaribisha Ziyech kwenye klabu
hiyo huku akimalizia kwa emoji ya tabasamu.
“Karibu Hakim,”
Olunga aliandika.
Ziyech alitambulishwa Alhamisi jioni
na klabu ya Ligi ya Qatar Stars baada ya kuondoka kwake kwa njia isiyo ya
kawaida kutoka Galatasaray.
"Al-Duhail Sports Club
ilifanikiwa kupata saini ya mchezaji wa kimataifa wa Morocco Hakim
Ziyech," taarifa ya Al
Duhail ilisema.
Winga huyo wa kulia mwenye umri wa
miaka 31 aliichezea timu ya taifa ya Uholanzi katika ngazi ya vijana na
atacheza chini ya bosi wa zamani wa Paris Saint-Germain Christophe Galtier.
Hapo awali alijiunga na Galatasaray
kwa mkopo kutoka Chelsea mnamo 2023 lakini alitofautiana na meneja Okan Buruk.
Mwezi uliopita, alisema hataki
kuichezea klabu hiyo tena katika ungamo la kikweli lililozua mjadala mkubwa Zaidi
kwenye ulimwengu wa soka duniani.
"Ukurasa Galatasaray umefungwa
kwangu. Sitaki tena kucheza hapa. Ninaondoka Januari,"
alinukuliwa na jarida na spoti la GOAL.
"Sijawahi kuona kocha wa kiwango
cha chini namna hii. Sijali sana [kama kujiunga na Galatasaray lilikuwa kosa].
Nataka kuachwa peke yangu, bila kujali kitakachotokea. Ninajuta kuja
hapa."
Olunga ambaye miezi michache
iliyopita aliweka rekodi kama mchezaji mwenye mabao mengi Zaidi katika historia
ya klabu ya Al Duhail amekuwa katika klabu hiyo tangu 2021 na kushinda taji la
2023.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30
pia alishinda viatu viwili vya Dhahabu vya Ligi ya Qatari Stars.
Sasa ataungana na Ziyech mshindi wa
Ligi ya Mabingwa akiwa na Chelsea. Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax alikuwa
sehemu ya timu ya Morocco iliyoshiriki Kombe la Dunia la 2022