Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, wamemteua Sinisa Mihic kuwa kocha wao mkuu mpya.
Uamuzi wa kumwajiri Mcroatia huyo mwenye umri wa miaka 48 ulifanywa wiki hii. Mihic aliwasili nchini mnamo Februari 1, tayari kutia sahihi kwa mkataba ambayo maelezo yake yatawekwa wazi atakapozinduliwa rasmi.
Mmiliki huyo wa leseni ya UEFA anachukua mikoba kutoka kwa kocha wa muda Zedekiah ‘Zico’ Otieno, ambaye alikuwa ameiongoza Gor Mahia kwa miezi mitatu pekee, kufuatia kutimuliwa kwa mtangulizi wake Leo Martins Neiva.
Tayari mashabiki wa K'Ogalo wameelezea kutoridhishwa kwao na utendakazi wa Zico ambaye amekumbana na changamoto katika kuorodhesha matokeo chanya.
Nafasi yake katika klabu bado haionekani, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba atasalia katika nafasi ya kocha msaidizi.
Mihic, ambaye muda wake wa umeneja katika vilabu ni wastani wa miaka 1.29, mara ya mwisho alihudumu kama kocha msaidizi wa klabu ya Al Salmiya SC ya Kuwait, na aliwahi kuwa kocha mkuu katika timu za daraja la tatu za Kroatia NK Crikvenica, Al Shabab - Kuwait, na Al-Fahaheel SC.
Hasa, Mihic ana uzoefu wa kufanya kazi barani Afrika, akiwa kama meneja msaidizi katika klabu ya Al-Merrikh ya Sudan mwaka 2009, kabla ya kuchukua nafasi kama hiyo kwenye Ligi Kuu ya Libya akiwa na Al Nasr mwaka wa 2010.