
Moraa akizungumza amewataka watu wanaomuunga mkono kumtakia mema anapoondoka nchini kuelekea Jamaika kwa ajili ya Mapambano ya Grand Slams Track.
"Niko tayari, leo nitakuwa naondoka nchini kuelekea nchini Jamaika. Mbio za kwanza msimu huu za Grand slam. Niko tayari kabisa. Licha ya kwamba ni pambano jipya kwangu. Inajumuisha mbio za mita 800 na mita 1500. Najua na kuelewa kwamba ni pambano gumu ila niko tayari," alisema Moraa.
Mkimbiaji huyo ameelezea imani kwamba atafanya vizuri licha ya changamoto zilizoko mbele yake na akawataka wakenya kusubiri matokeo.
"Naenda kung'ang'ania,. Kile naweza kuwaambia kwa sasa ni kwamba mngoje tu matokeo. Nimekuwa nikifanya mazoezi na kocha wangu, mwili wangu uko sawa. Lakini kujumuisha kwa hizo mbio zote ni changamoto kwangu. Lakini nitaenda kujikaza kadri ya uwezo wangu," aliongeza mwanariada huyo.
Bodi ya Watalii ya Jamaica (JTB) imeshirikiana na Grand Slam Track™ kuandaa hafla hiyo ya uzinduzi iliyopangwa kufanyika Kingston wiki hii kutoka Aprili 4-6. Grand Slam Track™ ni mashindano ya kitaalamu yaliyozinduliwa na Bingwa wa Olimpiki mara nne Michael Johnson.
Mapambano hayo yatajumuisha matukio makubwa ya michezo ya riadha na burudani za kiwango cha kimataifa.
Mji wa Kingston utakuwa mwenyeji wa kwanza kati ya mapambano manne ya Slams yanayotarajiwa.Michezo hiyo itahusisha wanariadha wenye kasi zaidi duniani.
Mashabiki watakaohudhuria wenye kasi na ustadi kutoka kwa Olimpiki na Mabingwa wa Dunia ni kama Gabby Thomas, Kenny Bednarek, Fred Kerley, na wengine wengi.
Washindani hao watakimbia mara mbili kwa siku tatu, wakishindana kwa dimbwi kubwa zaidi la pesa na zawadi kuwahi kutolewa katika mchezo huo.
Tukio hilo litatiririshwa moja kwa moja kwenye Peacock nchini Marekani, huku The CW ikitangaza matangazo ya Jumamosi na Jumapili ya Slams zote.