Ferdinand Omanyala: Kwa nini mtu mwenye kasi zaidi Afrika hakukatishwa tamaa na marufuku ya dawa aliyowekewa?

Muhtasari

•Omanyala ambaye alianza kazi yake ya riadha katika mwaka 2016, aliwekewa marufuku ya miezi 14 mwaka 2017 , baada ya vipimo kuonyesha kuwa alikuwa ametumia dawa za kututumua misuli michezoni, ambazo binafsi anasema zilikuwa ni dawa za kuondoa maumivu alizokuwa amemeza.

Ferdinand Omanyala
Ferdinand Omanyala
Image: HISANI

Ferdinand Omurwa Omanyala anaweza kuwa ndiye mwanaume mwenye kasi zaidi barani Afrika baada ya kuvunja rekodi ya bara la Afrika katika mbio za mita 100, lakini Mkenya huyo anakiri kuwa marufuku ya matumizi ya dawa za kututumua misuli michezoni aliyowekewa mwaka 2017 itaathiri mafanikio yake.

Alikimbia kwa kasi ya sekunde 9.77 katika mbio za Kip Keino Classic mjini Nairobi na kuvunja rekodi ya sekunde 9.85 iliyowekwa na raia wa Afrika Kusini Akani Simbine mwezi Julai.

"Wakati wote ninapokimbia mbio hizi za kasi, watu huzungumza, lakini kwangu mimi ni kwa ajili yangu- Sikimbii kwa ajili ya mtu mwingine ," Aliiambia BBC Afrika michezo, kijana huyu mwenye umri wa miaka 25.

Muda wake unamfanya kuwa mwanaume wa nane mwenye kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa, licha ya kumaliza mbio akiwa wa pili akimfuata Mmarekani Trayvon Bromell ambaye pia aliweka rekodi bora binafsi ya sekunde 9.76.

Image: GETTY IMAGES

Omanyala ambaye alianza kazi yake ya riadha katika mwaka 2016, aliwekewa marufuku ya miezi 14 mwaka 2017 , baada ya vipimo kuonyesha kuwa alikuwa ametumia dawa za kututumua misuli michezoni, ambazo binafsi anasema zilikuwa ni dawa za kuondoa maumivu alizokuwa amemeza.

"Nilihisi nilikuwa muathiriwa wa hali," alieleza. "Ilikuwa ni dawa ya kumaliza maumivu halafu ikageuka kuwa ilikuwa na steroid ndani, na masaibu hayo yamenifanya kuwa mtu niliye sasa ."

"Ilinipa uvumilivu, ikanifanya kuwa imara -kwasababu ni changamoto ambayo hakuna mwanariadha ambaye angependa kuipitia- na ni funzo kwamba hupaswi kutumia kitu chochote na haupaswi kumuamini mtu yeyote katika riadha."

"Imekuwa vigumu lakini ilinifanya niache yaliyopita nyuma. Tunasamehe, tunasahau na kusonga mbele. Mimi ni yule mtu ambaye anaishi maisha ya wakati huo. Imekuwa safari ngumu kuanzia mwaka 2016-majeraha, marufuku-lakini yote hayo ni mambo yaliyopita. Tunaandaa hali ya baadaye ."

'Hakuna ukomo katika uwezekano'

Ferdinand Omurwa Omanyala aliweka rekodi ya kitaifa nchini Kenya mara mbili kwa kushinda mita 100 katika Tokyo Olympiki
Ferdinand Omurwa Omanyala aliweka rekodi ya kitaifa nchini Kenya mara mbili kwa kushinda mita 100 katika Tokyo Olympiki
Image: GETTY IMAGES

Ferdinand Omurwa Omanyala aliweka rekodi ya kitaifa nchini Kenya mara mbili kwa kushinda mita 100 katika Tokyo Olympiki

Omanyala anasisitiza kuwa anaweza kukimbia kwa kasi hata zaidi na ameweka rekodi ya chini ya sekunde 9.70 kama lengo lake, mafanikio ambayo yamefikiwa tu na magwiji kama vile Usain Bolt wa Jamaica, na Yohan Blake na Mmarekani Tyson Gay.

Mchezaji huyo wa zamani wa raga aliyegeuka na kuwa mkimbiaji wa mbio za kazi za masafa mafupi-anaamini kuwa anaweza kukimbia hata kwa kasi kubwa zaidi kuliko hiyo, na labda kukaribia rekodi ya dunia ya Bolt ya sekunde 9.58.

"Hakuna ukomo katika uwezekano ," alitabasamu.

Msimu huu umekuwa wa mafanikio kwani ameweza kufuzu kwa michuano ya robo fainali katika mbio za mita 100 katika Olympiki za kwanza, huku akiweka rekodi mpya ya Kenya ya sekunde 10.00 , akiwa ni mmoja kati ya watu watano waliofanikiwa zaidi katika kipindi cha miezi saba iliyopita.

"Nimekuwa nikipata mafanikio katika kila mbio kwasababu nimekuwa nikikimbia katika mashindano mengi sana mwaka huu ," anasema. "Hilo ndilo nitakalolifanya mwaka ujao na nitaanza mapema labda mwezi Machi . Kwahiyo itakapofika Juni, tutegemee mida ya kasi sana ."

Matumaini ya kuhamasisha

Mwanariadha wa mbio fupi Mmarekani Justin Gatlin ana matumaini kwamba Afrika inaweza kutoa wanariadha wenye kasi zaidi duniani siku zijazo
Mwanariadha wa mbio fupi Mmarekani Justin Gatlin ana matumaini kwamba Afrika inaweza kutoa wanariadha wenye kasi zaidi duniani siku zijazo
Image: GETTY IMAGES

Katika nchi inayofahamika kwa kuwa na wanariadha bora katika mbio za masafa ya kati na masafa marefu, Omanyala sasa analenga kuhamasisha kizazi kijacho cha wanariadha wa masafa mafupi Wakenya.

"Ombi langu kubwa ni kwamba katika miaka mitano ijayo tuwe na akina Omanyala, watoto zaidi wanaoweza kukimbia mbio za masafa mafupi, kwasababu mimi ni wa kwanza ambaye nilijaribu kung'ang'ana kufika juu ,"anasema.

"Ninafahamu kuna watu wengi ambao wanaweza kukimbia kwa kasi, katika soka na raga, kwahiyo kama tutaweza kuwapata wakimbiaji wa mbio fupi 10, Kenya itakuwa imepata mafanikio.

"Sasa wanaamini inawezekana , kwasababu wengi wa watu waliokuwa wakiingia katika mbio hizi walikuwa wanakatishwa tamaa na wazazi wao au watu wengine wakisema 'huwezi kufika popote nchini Kenya kwa mbio za masafa mafupi'. Lakini sasa watu wanaamini hii inawezekana.

"Sasa ninataka kufungua klabu ya mbio za kasi za masafa mafupi na kuwatia moyo wakimbiaji vijana kufanya mazoezi na kuona ni wapi wanaweza kwenda."

Mwanaume mmoja anayeamini kwamba Omanyala, Simbine na Mnigeria kama Enoch Adegoke, aliyefikia finali ya Olympiki mita 100 watawatia moyo Waafrika wenzao ni Mshindi wa zamani wa Olympiki na dunia Justin Gatlin.

Mmarekani huyo, aliyemaliza nyuma kidogo ya Omanyala Jumamosi pia alielezea mafanikio ya Waafrka matika matukio ya viwanjani.

"Kipaji cha mbio za masafa mafupi za kazi katika Afrika ni kikubwa," aliimbia BBC.

"Dunia hinawaona wanariadha wa Afrika kama wakimbiaji wa mbio za masafa marefu tu , lakini sasa kuna warusha tufe, warukaji , wakimbiaji wa mbio za kasi za masafa mafupi , kwahiyo ninadhani imeonyesha duniakwamba inazaidi kuliko kipaji cha masafa marefu tu.

"Hicho ni kitu kikubwa kuwa nacho.Nimekuwa kila mara nikiamini kwamba Afrika ina mengi ya kutoa kwa dunia zaidi ya kile ilicho nacho tayari."

Wanaume wenye kasi zaidi katika historia:

  • Usain Bolt (Jamaica) - sekunde 9.58
  • Tyson Gay (Marekani) - sekunde9.69
  • Yohan Blake (Jamaica) - sekunde 9.69
  • Asafa Powell (Jamaica) - sekunde 9.72
  • Justin Gatlin (Marekani) - sekunde 9.74
  • Christian Coleman (Marekani) - sekunde 9.76
  • Trayvon Bromell (Marekani) - sekunde 9.76
  • Ferdinand Omanyala (Kenya) - Sekunde 9.77s
  • Nesta Carter (Jamaica) - sekunde 9.78
  • Maurice Greene (Marekani ) - sekunde 9.79