Mwanariadha Ferdinand Omanyala apokea zawadi ya gari baada ya kuvunja rekodi ya Afrika

Muhtasari

•Gwiji huyo wa mbio za mita 100 alipokea tuzo hilo baada ya kuvunja rekodi ya bara Afrika katika mbio hizo kwenye mashindano ya Kip Keino Classic siku ya Jumamosi.

•Omanyala alimaliza mbio hizo kwa sekunde 9.77, milisekunde moja tu nyuma ya mshindi Brommel.

•Omanyala alishukuru kampuni hiyo kwa kumsaidia katika safari yake ya riadha na kushauri wanariadha wenzake kutia bidii kubwa na kutokata tamaa kuhusiana na ndoto zao.

Image: TWITTER// ODIBETS

Mwanariadha Ferdinand Omanyala alitunukiwa gari mpya aina ya Toyota Harrier na kampuni ya kamari ya Odibets siku ya Jumatano.

Gwiji huyo wa mbio za mita 100 alipokea tuzo hilo baada ya kuvunja rekodi ya bara Afrika katika mbio hizo kwenye mashindano ya Kip Keino Classic siku ya Jumamosi.

Kwenye hafla hiyo ambayo ilifanyika katika hoteli ya New Stanley, meneja wa Odibets Dedan Mungai alisema kwamba kampuni yake inajivunia sana kushirikiana na Omanyala anapoendelea kung'aa.

Omanyala alishukuru kampuni hiyo kwa kumsaidia katika safari yake ya riadha na kushauri wanariadha wenzake kutia bidii kubwa na kutokata tamaa kuhusiana na ndoto zao.

Siku ya Jumamosi Omanyala alimaliza wa pili, nyuma ya Mmarekani Trayvon Brommel kwenye mashindano ambayo yalifanyika katika uwanja wa Kasarani.

Omanyala alimaliza mbio hizo kwa sekunde 9.77, milisekunde moja tu nyuma ya mshindi Brommel.

Gari ambalo Omanyala alipokea litakuwa na nambari 977 ili kusherehekea rekodi yake katika mbio hizo.

Hapo awali mwanariadha huyo alikuwa ametuzwa kwa shilingi milioni 1.5 na kampuni hiyo baada ya kuhitimu kushiriki kwenye mashindano ya Olimpiki Tokyo.1