Hongera! Eliud Kipchoge apokea tuzo ya mwanariadha bora wa kiume katika mashindano ya Tokyo Olympics

Muhtasari

•Kipchoge ambaye alikuwa ameteuliwa pamoja na wanariadha wengine tisa alipokea tuzo hilo kwenye hafla iliyofanyika jijini Creek nchini Greek siku ya Jumapili.

•Kipchoge alipokea tuzo hilo baada ya kunyakua dhahabu ya mbio za Marathon katika Olimpiki  kwa mara ya pili mfululizo.

Image: TWITTER// ELIUD KIPCHOGE

Eliud Kipchoge ameendelea kutambuliwa kutokana na ubabe wake kwenye ulingo wa riadha huku sasa akipokea tuzo la mwanariadha bora wa kiume katika mashindano ya Tokyo Olympics yalifanyika mapema mwakani.

Kipchoge ambaye alikuwa ameteuliwa pamoja na wanariadha wengine tisa alipokea tuzo hilo kwenye hafla iliyofanyika jijini Creek nchini Greek siku ya Jumapili.

Kipchoge alisema kwamba anajivunia sana kutambuliwa kama mwanariadha bora kati ya wengi waliofanya vizuri huku akiwashuru wote ambao wamemuunga mkono katika taaluma yake.

"Ni furaha kushinda tuzo la ANOC la mwanariadha bora wa kiume katika mashindano ya Tokyo Olympics. Kati ya maonyesho mazuri ya wanariadha wengi, najivunia kuwa mwenye kunyakua tuzo hili. Shukran nyote kwa kuendelea kuniunga mkono" Kipchoge aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kipchoge alipokea tuzo hilo baada ya kunyakua dhahabu ya mbio za Marathon katika Olimpiki  kwa mara ya pili mfululizo. Hapo awali alikuwa amenyakua ushindi katika mashindano ya Rio Olympics mwaka wa 2016.

Kwenye mashindano ya Tokyo Olympics 2022 ambayo yalifanyika nchini Japan mwaka huu, Kipchoge aliibuka mshindi baada ya kukimbia kwa masaa mawili, dakika nane na sekunde 38.

Mwogeleaji Margaret MacNeil kutoka Canada alinyakua tuzo la mwanariadha bora wa kike baada ya kushinda medali tatu katika mashindano ya Tokyo Olympics.