Omanyala avunja rekodi ya mita 60 kwa mara ya 3 nchini Ufaransa

Muhtasari

• Ferdinand Omanyala ameandikisha rekodi mpya katika mbio za mita 60 kwa mara ya tatu mtawalia katika mbio zilizoandaliwa Ufaransa, Februari 17

Ferdinand Omanyala
Ferdinand Omanyala
Image: HISANI

Mwanariadha Ferdinand Omanyala kwa mara nyingine tena amepeperusha bendera ya Kenya kwa madoido mno baada ya kuvunja rekodi ya mita sitini kwa mara ya tatu sasa katika mbio zilizoandaliwa nchini Ufaransa, Februari 17.

Omanyala ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa mwanamme mwenye mbio Zaidi barani Afrika kwa mara nyingine tena alipunguza rekodi ya kitaifa katika mbio za mita 60 kwa mara ya tatu mtawalia kwenye mashindano yaliyoandaliwa Assembly Hauts-de-France Pas-de-Calais huko Lievin nchini Ufaransa.

Katika mbio hizo, Omanyala aliandikisha rekodi ya sekunde sita nukta tano saba (6.57) na kumaliza wa nne nyuma ya Muitaliano Jacobs Marcell aliyeshinda mbio hizo kwa sekunde 6.50 akifuatiwa na Mmarekani Cravont Charleston (6.52) katika nafasi ya pili na mwenzake Elijah Corridor (6.57) kutokea Marekani pia akawa wa tatu mbele ya Omanyala.

Hii ni mara ya tatu ambapo Omanyala, 26, aliandikisha rekodi mpya kwenye mbio hizo baada ya kufanya hivo Februari 4, miezi michache tu baada ya kuvunja rekodi iliyokuwa imewekwa miaka 17 iliyopita.

Hongera sana Omanyala!