Natumai hautaacha kuja kutazama mbio zangu - Omanyala amwambia rais Kenyatta

Asante kwa huduma yako - Omanyala

Muhtasari

• Rais Kenyatta amekuwa akihudhuria mashindano ya mbio za Omanyala katika viwanja mbali mbali nchini.

Omanyala amtakia rais Kenyatta heri njema ya kustaafu
Omanyala amtakia rais Kenyatta heri njema ya kustaafu
Image: Facebook

Mwanariadha wa mbio za mita 100, Ferdiand Omanyala amemtakia rais mstaafu Uhuru Kenyatta heri njema katika maisha yake ya baada ya urais.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Omanyala alimtaka Kenyatta kutokoma kuenda katika uwanja wa mashindano ili kumshuhudia akitimuka kama ilivyokuwa kawaida yake.

“Heri njema ya kustaafu..... natumai hautaacha kuja kutazama mbio zangu. Asante kwa huduma yako,” Omanyala aliandika kwa hisia mno.

Ikumbukwe mapema mwaka huu katika uga wa Kasarani, Uhuru alihudhuria mashindano ya Kipchoge Keino Classic ambapo alishuhudia mwanariadha huyo akitimuka na kummiminia sifa tele kwamba ameibeba bendera ya Kenya katika mbio za mita mia moja hata Kwenda katika mashindano ya dunia.

Miezi miwili iliyopita wakati visa ya kusafiria ya Omanyala ilikumbwa na utata mpaka kumfanya kuchelewa kusafiri marekani kushiriki mashindano ya Oregon, rais Uhuru Kenyatta aliingilia kati na kuhakikisha Omanyala amesafiri japo muda ulikuwa umeyoyoma.