FURAHA TELE

Chepngetich na Kipruto watwaa mataji ya Chicago Marathon

Kipruto, 31, alimaliza mbio hizo kwa saa 2:04.24 na kurejesha taji alilopoteza Aprili mwaka jana.

Muhtasari

•Katika mbio za wanawake, Mkenya Ruth Chepng'etich alihifadhi taji lake.

•Chepng'etich alirekodi muda bora wa binafsi wa 2:14:18, huku akikosa rekodi ya dunia kwa sekunde 14.

Ruth Chepng'etich
Ruth Chepng'etich
Image: HISANI

Mkenya Benson Kipruto ndiye bingwa wa mwaka huu wa Chicago Marathon baada ya kufutilia mbali safu kali ya washindani kushinda mbio hizo siku ya Jumapili.

Kipruto, 31, alimaliza mbio hizo kwa saa 2:04.24 ili kurejesha taji alilopoteza Aprili mwaka jana.

"Nina furaha kushinda na kuweka PB mpya. pia nina furaha kuweka taji katika familia. Kozi hapa ni tambarare na huu ni mji mzuri," Kipruto alisema baada ya ushindi wake.

Bingwa mtetezi Seif Tura wa Ethiopia alimaliza wa pili kwa 2:04:49 huku bingwa wa Los Angeles Marathon John Korir akimaliza wa tatu kwa 2:05:01.

Katika mbio za wanawake, Mkenya Ruth Chepng'etich alihifadhi taji lake.

Chepng'etich alirekodi muda bora wa binafsi wa 2:14:18, huku akikosa rekodi ya dunia kwa sekunde 14.

Rekodi hiyo iliwekwa na mzalendo Brigid Kosgei kwenye Chicago Marathon mwaka wa 2019.

Emily Sisson wa Marekani alikuwa wa pili kwa saa 2:18:20 huku Vivian Kiplagat akimaliza wa tatu kwa 2:20:52.

Mkenya Bornes Jepkirui alishinda mbio za Lisbon Marathon kwa 2:24:17. Waethiopia Sorome Negash na Buzunesh Getachew walimaliza wa pili na wa tatu kwa 2:25:57 na 2:26:01 mtawalia. Mkenya mwingine Jane Jelagat alimaliza wa saba kwa 2:30:34.

Katika mbio za wanaume, Waethiopia walichukua nafasi tatu za kwanza kupitia Andualem Belay, Haftu Teklu na Birhan Nebew waliotumia saa 2:05:45, 2:06:33 na 2:07:04.

Mkenya Julius Kipkorir alimaliza wa nne kwa 2:08:23. Wakenya wengine katika mbio hizo walikuwa Paul Eyanae na Nicholas Kirwa walioshika nafasi za nane na tisa katika muda wa 2:13:46 na 2:14:31 mtawalia.

Katika mbio za Munich Marathon, Philemon Kipchumba na Agnes Keino walishinda mbio za wanaume na wanawake kwa saa 2:07.28 na 2:23.26 mtawalia.

Mengistu Gezahagn wa Ethiopia na Mueritrea Berhane Tesfay walishika nafasi ya pili na ya tatu nyuma ya Kipchumba katika mbio za wanaume.

Wakenya wengine Edwin Kimaiyo, Rodgers Keror, Meshack Koech na Vincent Kiprotich walimaliza katika nafasi za tano, sita, saba na tisa mtawalia.

Katika mbio za wanawake, Marr Hurssa wa Ethiopia na Souad Kanbouchia wa Morocco walitumia 2:24:12 na 2:27:35 kumaliza wa pili na wa tatu.

Wakenya wengine Viola Yator na Helen Jepkurgat walipata nafasi ya nne na nafasi ya saba baada ya kumaliza kwa muda wa 2:28.11 and 2:32.07 mtawalia.