MARUFUKU

Mwanariadha wa Kenya ajipata matatani

AIU imempiga marufuku mwanariadha wa mbio za marathoni Philemon Lokedi kwa kuvunja sheria.

Muhtasari

•Kando na kufuta matokeo ya Lokedi tangu Aprili 27, AIU ilitoa adhabu nyingine ikiwa ni pamoja na kupokonywa mataji, tuzo, medali, zawadi na ada za kuonekana.

•AIU ilithibitisha kwamba marufuku yake Lokedi ilipunguzwa kwa mwaka mmoja baada ya kukiri ukiukaji huo.

Mwanariadha Philemon Lokedi
Mwanariadha Philemon Lokedi
Image: HISANI

Kitengo cha Uadilifu cha Riadha (AIU) kimempiga marufuku mwanariadha wa Kenya Philemon Kacheran Lokedi kwa miaka mitatu baada ya sampuli yake kuthibitishwa kuwa na Testosterone.

Lokedi, 30, alikuwa amechaguliwa kupeperusha bendera ya Kenya katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Birmingham 2022 nchini Uingereza, lakini nafasi yake ikachukuliwa dakika za mwisho na mshindi wa medali ya shaba Michael Githae.

Wanakikundi wengine walikuwa Eric Kiptanui na Jonathan Korir.

Mwanariadha huyo alifanyiwa majaribio sampuli yake mjini Kapenguria mnamo Aprili 27. Marufuku hiyo imerejeshwa nyuma hadi Julai 8, 2022.

AIU ilithibitisha kwamba marufuku yake Lokedi ilipunguzwa kwa mwaka mmoja baada ya kukiri ukiukaji huo.

Kando na kufuta matokeo ya Lokedi tangu Aprili 27, AIU ilitoa adhabu nyingine ikiwa ni pamoja na kupokonywa mataji, tuzo, medali, zawadi na ada za kuonekana.

Lokedi alipaswa kuwakilisha Kenya katika Riadha Ulimwenguni huko Oregon, Marekani mwezi Juni.

Alimaliza wa tatu katika mbio za marathon za Valencia kwa saa 2:05.19 Desemba iliyopita.