Usain Bolt aripotiwa kuibiwa mamilioni ya pesa kutoka kwa akaunti yake kwa ulaghai

Taarifa zinasema kuwa mamlaka ya kusimamia fedha Jamaica imeanzisha uchunguzi baada ya pesa zake nyingi kutowekwa kutoka kwa akaunti yake.

Muhtasari

• Bolt ndio mshikilizi wa rekodi bora katika mbio za mita 100 na 200 ambazo aliweka miaka zaidi ya 10 iliyopita.

Usain Bolt anahofiwa kupoteza mamilioni ya pesa kwa ulaghai
Usain Bolt anahofiwa kupoteza mamilioni ya pesa kwa ulaghai
Image: Facebook

Mwanariadha mshikilizi wa rekodi za dunia katika mbio za mita 100 na mita 200, Usain Bolt kutoka Jamaica anaripotiwa kupoteza mamilioni ya pesa kupitia ulaghai mkubwa.

Kulingana na jarida la AFP, mamlaka inayosimamia fedha nchini Jamaica imeanzisha uchunguzi dhidi ya kampuni ya kuwekeza pesa ambayo Bolt alikuwa amewekeza pesa zake na ambazo zimeofiwa kutoweka kwa njia za ulaghai.

Meneja wa Bolt Nugent Walker aliliambia gazeti la Jamaica Gleaner kwamba mwanariadha huyo aliyestaafu, mmoja wa wanariadha wakubwa wa wakati wote, amekuwa na uwekezaji na kampuni hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.

"Hatua zote muhimu zimechukuliwa ili kufafanua jambo hili," Walker aliambia jarida hilo, akisema mwanariadha huyo aligundua hitilafu na akaunti yake siku ya Jumatano.

"Amekuwa mteja wa kampuni hii kwa zaidi ya miaka 10...," aliongeza.

Gazeti hilo lilisema mamilioni ya dola yaliripotiwa kupotea kwenye akaunti ya Bolt.

Bolt alistaafu kutoka kwa riadha mnamo 2017 baada ya taaluma nzuri ambayo pamoja na medali nane za dhahabu za Olimpiki zilijumuisha medali 11 za dhahabu za Ubingwa wa Dunia.

 

Bolt alijizolea umaarufu duniani katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka wa 2008 aliposhinda mbio za mita 100 na 200, akiweka rekodi mpya za dunia katika mbio zote mbili.

Mjamaika huyo aliendelea kushinda mbio zote mbili katika Michezo ya London ya 2012 na Rio 2016.

Miaka zaidi ya saba tangu kustaafu mbio, rekodi zake katika mita 100 na mita 200 bado zinasalia kama rekodi bora na hakujatokea mwanariadha mwingine wa kuzipiku.