Shirika la riadha duniani limepiga marufuku wanawake waliobadili jinsia kushiriki mashindano ya viwango vya kimataifa vya wanawake

Rais Lord Coe, alisema hakuna mwanariadha aliyepitia balehe ya kiume na kubadili jinsia atakayeruhusiwa kushiriki kama wanawake.

Muhtasari

• Rais Lord Coe alibainisha kuwa kwa sasa hakuna wanariadha waliobadili jinsia wanaoshiriki mashindano ya kimataifa katika mchezo huo.

Rais wa shirika la riadha duniani Lord Coe, alisema hakuna mwanariadha aliyebadili jinsia ambaye amepitia balehe ya kiume ataruhusiwa kushiriki katika mashindano ya viwango vya dunia ya wanawake kuanzia tarehe 31 Machi.

Kikundi cha kazi kitaundwa ili kufanya utafiti zaidi katika miongozo ya stahiki kwa watu waliobadili jinsia. "Hatusemi kuwa tutakataa milele," alisema.

Chini ya sheria za awali, shirika la riadha la dunia liliwataka wanawake waliobadili jinsia kupunguza kiwango chao cha homoni za kiume hadi kiwango cha juu cha 5nmol/L, na kukaa chini ya kiwango hiki kwa mfululizo wa muda wa miezi 12 kabla ya kushindana katika kitengo cha wanawake.

Bwana Lord Coe aliongeza uamuzi huo "unaongozwa na kanuni kuu ambayo ni kulinda jamii ya wanawake".

Alibainisha kuwa kwa sasa hakuna wanariadha waliobadili jinsia wanaoshiriki mashindano ya kimataifa katika mchezo huo.

“Maamuzi huwa magumu kila mara yanapohusisha mahitaji na haki zinazokinzana kati ya makundi mbalimbali, lakini tunaendelea kuchukua mtazamo kwamba ni lazima tudumishe haki kwa wanariadha wa kike zaidi ya mambo mengine,” alisema Lord Coe.

"Tutaongozwa na sayansi katika utendaji wa hili kuhusu masuala ya mwili na faida ya kiume ambayo itakua kwa miaka ijayo. Ushahidi zaidi unapatikana, tutapitia msimamo wetu, lakini tunaamini uadilifu wa kitengo cha wanawake katika riadha ni muhimu. .

"Baraza lilikubali kuanzisha kikosi kazi kwa muda wa miezi 12 "kuangazia zaidi suala la ujumuishaji wa watu waliobadili jinsia".

Mwenyekiti wa kujitegemea ataongoza kundi hilo, huku pia litajumuisha hadi wajumbe watatu wa baraza, wanariadha wawili kutoka Tume ya Wanariadha, mwanariadha aliyebadili jinsia, wawakilishi watatu wa mashirikisho wanachama wa Riadha Duniani na wawakilishi wa idara ya afya na sayansi ya Riadha Duniani.

Itashauriana haswa na wanariadha waliobadili jinsia, na pia kupitia na kuagiza utafiti na kutoa mapendekezo kwa Baraza.