Mwanariadha wa Kenya Faith Kipyegon alivunja rekodi ya mbio za mita 1500 upande wa wanawake siku ya Ijumaa wakati wa mashindano ya Diamond League, jijini Florence nchini Italia.
Kipyegon aliweka rekodi mpya ya dakika 3 na sekunde 49.11, akivunja rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Genzebe Dibaba wa Ethiopia ambaye alikuwa amekimbia kwa dakika 3 na sekunde 50.07 mwaka wa 2015. Kipyegon alivuka rekodi ya Dibaba kwa sekunde 0.96.
Akizungumza baada ya mbio hizo, Kipyegon alieleza furaha yake kubwa kwa ushindi huo na kukiri kuwa hakutarajia kuvunja Rekodi ya Dunia.
"Nimefurahi sana, nina furaha sana, sikutarajia hili. Nilitarajia uongozi wa dunia, sio rekodi ya dunia, lakini ninashukuru sana.. Kama nilivyosema leo na jana kila kitu kinawezekana," Kipyegon alisema. katika mahojiano na mtangazaji wa RAI.
Laura Muir wa Scotland aliibuka wa pili kwa rekodi ya dakika 3 na sekunde 57.09 huku Jessica Hull wa Australia akichukua nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa dakika 3 na sekunde 57.29.
Faith Kipyegon ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 29 amekuwa akishiriki mashindano ya kimataifa kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa baada ya kuanza taaluma yake ya riadha akiwa na umri mdogo.
Sasa anajiunga na orodha ya wanariadha wengine Wakenya wanaoshikilia rekodi ya dunia katika mbio mbalimbali wakiwemo Eliud Kipchoge, David Rudisha, Brigid Kosgei, Beatrice Chepkoech na Agnes Tirop wanaoshikilia rekodi katika marathoni ya wanaume, mbio za mita 800 za (wanaume), marathon (wanawake), mita 3000 (wanawake) mbio za kuruka viunzi za kilomita 10 (wanawake) mtawalia.