Mwanariadha Faith Kipyegon avunja rekodi ya 3 ya dunia ndani ya miezi miwili

Siku ya Ijumaa jioni, Kipyegon alivunja Rekodi ya Dunia ya Maili ya wanawake katika Monaco Diamond League.

Muhtasari

•Kipyegon alitumia muda wa dakika 4:07.64, na kuvunja rekodi ya miaka minne ya Sifan Hassan ya  dakika 4:12.33 katika maili ya wanawake.

• Kipyegon aliweka rekodi ya mita 1500 kwenye Florence Diamond League mnamo Juni 2, 2023 kabla ya kutinga nyingine katika mbio za mita 5000 jijini Paris wiki moja baadaye.

amevunja rekodi ya tatu ndani ya miezi miwili
Faith Kipyegon amevunja rekodi ya tatu ndani ya miezi miwili
Image: HISANI// NIKE

Bingwa wa Olimpiki Faith Kipyegon ameongeza taji lingine na kuvunja rekodi nyingine ya dunia.

Siku ya Ijumaa jioni, Kipyegon alivunja Rekodi ya Dunia ya Maili ya wanawake katika Monaco Diamond League.

Alitumia muda wa dakika 4:07.64, na kuvunja rekodi ya miaka minne ya Sifan Hassan ya  dakika 4:12.33 katika maili ya wanawake.

Anakuwa mwanamke wa kwanza kukimbia kwa chini ya dakika 4:10 katika maili na sasa amevunja Rekodi tatu za Dunia katika mwaka wa 2023 pekee."

Rekodi nyingine za dunia alizovunja ni katika mbio za mita 1500 na 5000.

 Kipyegon aliweka rekodi ya mita 1500 kwenye Florence Diamond League mnamo Juni 2, 2023 kabla ya kutinga nyingine katika mbio za mita 5000 jijini Paris wiki moja baadaye.

Rais William Ruto alimpongeza kwa ushindi huo akisema ameifanya Kenya kujivunia.

"Rekodi nyingine ya Dunia imevunjwaa. Kipaji kisicho na kifani cha Faith Kipyegon, ukakamavu wa hali ya juu na uchezaji wa hali ya juu umeangaza ulimwengu tena wakati huu katika mashindano ya 1-Mile Monaco Grand Prix. Kenya inasherehekea Faith kwa kuwa miongoni mwa wanariadha bora zaidi katika maisha yetu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa upande wake alisema:

"Faith Kipyegon ni yeye! Hongera kwa kuweka rekodi ya 4:07.64 na kuvunja Rekodi ya Dunia ya Maili Moja kwenye Ligi ya Diamond ya Monaco.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alimtaja kama msukumo.

"Hongera Faith Kipyegon kwa kuvunja rekodi ya dunia ya maili moja. Wewe ni msukumo wa kweli. Endelea kung'aa !" alisema.