'Sioni hili likibadilika' - Saudia kuendelea kumwaga pesa kuwanunua wachezaji

Kupanda kwa Ligi ya Saudia kumelinganishwa na Ligi ya China iliyotumia pesa nyingi, na umaarufu ukashuka baada ya kuanza kwa kasi.

Muhtasari

•"Bajeti ya matumizi ipo miaka kadhaa - sioni hela ya ikipungua hivi karibuni," mkurugenzi wa Uingereza Peter Hutton alisema.

•Saudi Arabia imewekeza fedha nyingi katika michezo katika miaka ya hivi karibuni na imeshutumiwa kwa kutumia michezo hiyo 'kusafisha' sifa yake.

Image: BBC

Matumizi ya "ajabu" ya Ligi ya Saudia Pro kuwanunua wachezaji yanatarajiwa kuendelea, kulingana na mmoja wa wasimamizi wake wakuu.

"Bajeti ya matumizi ipo miaka kadhaa - sioni hela ya ikipungua hivi karibuni," mkurugenzi wa Uingereza Peter Hutton, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa bodi ya ligi hiyo alisema.

SPL imewavutia baadhi ya wachezaji wakubwa wa soka tangu mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or Cristiano Ronaldo alipojiunga Januari akitokea Manchester United.

Wengine waliojiunga na ligi hiyo ni pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema, nahodha wa zamani wa Liverpool Jordan Henderson na wachezaji mahiri kutoka Chelsea, Manchester City na Bayern Munich.

Mwezi uliopita Al-Hilal walitoa ofa iliyoweka rekodi ya dunia ya £259m kumnunua mshambuliliaji wa Paris St-Germain Kylian Mbappe.

Hutton, ambaye amekuwa mtendaji mkuu katika Eurosport, ESPN, IMG na Facebook, alisema: "Nimefanya kazi katika nyanja ya michezo kwa miaka 40 na sijawahi kuona mradi mkubwa, wenye ari na nia ya kufanikiwa. "

Akizungumza na mhariri wa michezo wa BBC Dan Roan katika mahojiano mapana ya kipindi maalum cha 'The Saudi Story' katika kituo cha BBC Radio 5 Live , alisema "si lazima iwe jambo baya" ikiwa soka la Ulaya halina nguvu kama ilivyokuwa.

Hutton pia aliweka matumizi ya Saudi katika muktadha, akisema "matumizi ya ligi ya Saudia imezua gumzo katika ulimwengu wa michezo lakini ni robo au tusui ya fedha ambazo zimetumiwa na vilabu vya Ligi Kuu msimu huu wa joto".

Kocha wa City Pep Guardiola amesema uwezo wa kifedha wa Ligi ya Saudia "umebadilisha soko" la uhamisho wa wachezaji na vilabu vikuu vya soka "vinahitaji kufahamu kinachoendelea", huku mwenzake wa Liverpool Jurgen Klopp akielezea wasiwasi wake kuhusu kufungwa kwa dirisha la uhamisho huko Saudi Arabia. .

Kulingana na Transfermarkt, vilabu vya SPL vimetumia euro milioni 409 kufikia sasa msimu huu wa joto - ya tano kwa matumizi ya juu katika kandanda duniani na zaidi ya euro 254m ya La Liga ya Uhispania (£218m). Ligi Kuu ya Primia inaongoza kwa kutumia euro bilioni 1.37.

Alipoulizwa jinsi Ligi Kuu ya Saudia ni tishio kubwa kwa mataifa yenye nguvu katika soka, Hutton alisema: "Uwekezaji wa Saudia ni wa ajabu. Hakika umekuwa kwa kasi kubwa.

"Hii haimaanishi kuwa Ulaya haitakuwa na nguvu katika soka la dunia. Lakini naweza kusema hilo si jambo baya. Ni vyema soka lina nguvu kote duniani."

Hoja ya 'kujitakasa kimichezo'

Saudi Arabia imewekeza fedha nyingi katika michezo katika miaka ya hivi karibuni na imeshutumiwa kwa kutumia michezo hiyo 'kusafisha' sifa yake.

Kuna hofu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na haki za wanawake nchini humo, wakati mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Saudi Arabia, huku adhabu ya kifo ikiwezekana kuzingatiwa.

Kujiunga kwa Henderson na klabu ya Al-Ettifaq kulikosolewa kutokana na uungwaji mkono wake wa awali wa jumuiya ya LGBTQ+.

Akijibu masuala haya, Hutton alisema: "Sababu iliyonifanya nijihusishe na KSA [Ufalme wa Saudi Arabia] ni kwamba niliona uhalisia wa baadhi ya mambo yaliyokuwa yakifanyika nchini.

"Mke wangu anafanya kazi katika soka la wanawake la Fifa, alikuwa anafahamu kile kinachofanyika katika ufalme. Na unashuhudia mabadiliko hayo, unaona jinsi inavyofurahisha jamii ya eneo hilo.

"Mabadiliko katika nafasi ya wanawake katika jumuiya ya Saudia ni ya ajabu na yanakuwa kwa kasi sana. Ni wazi machoni mwa mataifa ya Magharibi inaweza kusonga kwa kasi zaidi, lakini imesonga kwa kasi ya kushangaza katika muktadha wa historia ya ufalme huo.

“Naangalia ushahidi ninaouona sasa hivi umepata wasichana 50,000 wa shule wanaocheza soka, umepata makocha wanawake 1,000, mwaka 2018 makocha waliosajiliwa walikuwa 750, sasa wako zaidi ya 5,500.

"Kwa hivyo hatua hiyo ni kama ushahidi wa mabadiliko, na maendeleo ya soka ya wanawake ni kama sehemu ya mabadiliko ya jamii. Hiyo kwangu ndiyo kivutio cha kweli cha mradi huu.

"Sio tu kuhusu wachezaji wakuu na ada kubwa za uhamisho na mishahara. Pia inahusu miundombinu yote ya soka ya Saudia, iwe ya wanawake, soka la vijana, na msingi nzima ambayo unabadilisha mchezo nchini."

'Vilabu vya kweli vilivyo na mashabiki halisi'

Kupanda kwa Ligi Kuu ya Saudia kumelinganishwa na Ligi Kuu ya China iliyotumia pesa nyingi, na umaarufu wake kushuka baada ya kuanza kwa kasi.

Hazina ya Kitaifa ya Uwekezaji (PIF) imechukua usimamizi wa vilabu vinne vilabu vikuu vya SPL, huku kukiwa na kituo kimoja cha kununua wachezaji.

Hutton anaamini kuhusika kwa serikali katika SPL kunaweza kuwa kielelezo kwa nchi nyingine katika suala la kuleta pamoja vyuo vya soka, ligi ya wanawake, ligi ya wanaume na shirikisho la soka ili "kuunda ramani ya ukuaji ambayo inawiana, sio watu wanaopigania vitengo vyao".

"Ligi ya Saudi inajivunia utamaduni wa miaka 50. Ina mashabiki halisi na vilabu vilivyostawishwa. Haya ni mashindano ya kweli ambayo tunajaribu kuboresha badala ya kuanzisha kitu kipya," anasema Hutton.

"Jambo zuri kuhusu dau la Mbappe na usajili kama wa Ruben Neves inaonyesha sio wachezaji wa zamani tu wanaoangaziwa, Ni swali zaidi la nini kitaongeza thamani, nini kitaongeza uzuri, nini kitaongeza ubora wa ligi.

"Kuna vilabu halisi vilivyo na mashabiki wa kweli ambao wana msisimko wa kweli, kama vile mashabiki wa Chelsea au mashabiki wa Manchester City walivyofurahi wakati nyota walipojiunga na vilabu vyao. Kwetu pia sio tofauti sana."

Manufaa ya kibiashara

Alipoulizwa ni lini anatarajia ligi kupata faida kwa uwekezaji wake mkubwa, Hutton anasema: "Naweza kukadiria mapato makubwa sana katika muda wa miaka tisa au 10.

"Cha msingi ni kupta ongezeko la mwaka hadi mwaka na bila shaka matumaini ya kupata faida ya juu, mapato kutokana na matangazo ya TV yanaongezeka, udhamini umeongezeka. Sioni kwa nini hilo lipunguze.

"Ronaldo aliposaini Al Nassr ghafla tulivutia watangazaji wa kimataifa. Mwaka jana, tuliishia katika maeneo zaidi ya 170 mara tu Ronaldo aliposaini.

"Ni wazi ni jambo ambalo limevutia mawazo ya watangazaji kote duniani na hiyo imekuwa ishara chanya. Nina na imani kwamba tutapata mpango wa matangazo nchini Uingereza kwa msimu huu ujao."