Budapest: Wakenya Faith Kipyegon, Chebet, Kasait na Chelimo wafuzu kwa fainali ya mita 5,000

Kipyegon alisema ana furaha kuwa Wakenya wote wamefuzu na anatarajia fainali hiyo kuwa na ushindani mkubwa.

Muhtasari

•Wote walihitimu kwa fainali ya mbio za mita 5,000 baada ya kukimbia vizuri katika mbio za nusu fainali katika Uwanja wa Kitaifa mjini Budapest.

• Faith Kipyegon alitumia dakika 14:32.31 na kushika nafasi ya pili nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi ambaye alikimbia kwa dakika 14:32.29.

Faith Kipyegon
Faith Kipyegon
Image: HISANI

Wanariadha wa Kenya ya Faith Kipyegon, Beatrice Chebet, Lilian Kasait na Margaret Chelimo wote walihitimu kwa fainali ya mbio za mita 5,000 baada ya kukimbia vizuri katika mbio za nusu fainali katika Uwanja wa Kitaifa mjini Budapest.

Chebet alishinda katika kundo lake baada ya kukimbia kwa dakika 14:57.70 mbele ya Gudaf Taegay wa Ethiopia ambaye alitumia dakika 14:57.72 na Mkenya Margaret Chelimo akaibuka wa tatu kwa dakika 15:00.10.

Katika kundi la pili la nusu fainali, Faith Kipyegon alitumia dakika 14:32.31 na kushika nafasi ya pili nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi ambaye alikimbia kwa dakika 14:32.29.

Waethiopia wawili Ejgayehu Taye (14:33.23) na Freweyni Hailu (14:34.16Q) walishika nafasi ya tatu na nne mtawalia huku Kasait (14:36.61) akifunga nafasi tano za juu.

Katika mahojiano, Kipyegon alisema ana furaha kuwa Wakenya wote wamefuzu na anatarajia fainali hiyo kuwa na ushindani mkubwa.

Chebet alisisitiza maoni hayo hayo akisema fainali itashirikisha wakimbiaji bora wa sasa katika mashindano hayo.