Mamilioni ya pesa ambazo mshindi wa Chicago Marathon Kelvin Kiptum alichukua nyumbani

Kwa hesabu ya haraka, Mkenya huyo alitia mfukoni kitika cha zaidi ya shilingi za Kenya milioni 27 kwa kukimbia tu kwa saa mbili pekee!

Muhtasari

• Kando na tuzo hizo za pesa kutoka kwa waaandaji wa Chicago Marathon, serikali ya Kenya pia ilitimiza ahadi yake kwa kumpa Kiptum hundi ya shilingi milioni 5 Jumanne.

Kelvin Kiptum
Kelvin Kiptum
Image: HISANI

Ilikuwa siku ya kuvunja rekodi katika mbio za Chicago Marathon za 2023 zilizoongozwa na Mkenya Kelvin Kiptum, ambaye alivunja rekodi ya dunia, akitumia saa 2:00:35.

Muda wa kumaliza wa mwanariadha mwenye umri wa miaka 23 ulipita alama ya awali ya 2:01:09, iliyoshikiliwa na nguli wa mbio za marathoni Eliud Kipchoge, kwa sekunde 34; Kipchoge, wa Kenya, aliweka alama hiyo kwenye mbio za Berlin Marathon za 2022.

"Nilijua ninakuja kwa rekodi ya kozi, lakini kwa bahati nzuri, rekodi ya ulimwengu," Kiptum alisema baada ya mbio.

Bingwa mtetezi wa mbio za Chicago Marathon Benson Kipruto wa Kenya alimaliza wa pili kwa saa 2:04:02 naye Bashir Abdi wa Ubelgiji akashika nafasi ya tatu kwa saa 2:04:32.

Lakini je, baada ya ushindi huu, ni kima cha shilingi ngapi ambazo Mkenya huyo alikabidhiwa?

Kwa mujibu wa jarida la Sportico, Kiptum alitwaa tuzo ya pesa ya mshindi wa kwanza ya shilingi za Kenya milioni 14.89, na mwanariadha huyo anayedhaminiwa na Nike pia alipata bonasi ya shilingi milioni 7.45 kwa kuweka rekodi ya kozi (na dunia). Jumla ya pochi ya Chicago ya $560,000 imegawanywa sawasawa kati ya wanaume na wanawake.

Kando na tuzo hizo za pesa kutoka kwa waaandaji wa Chicago Marathon, serikali ya Kenya pia ilitimiza ahadi yake kwa kumpa Kiptum hundi ya shilingi milioni 5 Jumanne.

Hii inafuatia tangazo la rais Ruto mapema mwaka huu kwa Mkenya yeyote ambaye angeshinda na kuvunja rekodi yoyote duniani atapewa zawadi ya shilingi milioni 5.

Kiptum alikimbia katika mfano wa viatu vya Nike Alphafly 3, toleo ambalo litapatikana kwa umma mnamo 2024, kulingana na Habari za Viatu.